Moto nchini Ugiriki umesababishwa na nani? | Magazetini | DW | 27.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Moto nchini Ugiriki umesababishwa na nani?

Tangu siku tatu Ugiriki inakabiliwa na moto mkubwa katika sehemu mbali mbali ambao umewaua watu wasiopungua 60. Juu ya kuwa na wasiwasi juu ya athari za moto huo, raia wa Ugiriki wanazidi kuwa na hasira dhidi ya serikali yao.

Moto nchini Ugiriki

Moto nchini Ugiriki

Wanasiasa wanalaumiwa kutoweza kupambana na hatari hiyo, aidha wanaaminika kubeba dhamana fulani kwa kuzuka kwa moto huo. Wagiriki wengi wanaamini kuwa moto huo umesababishwa na wafanyabiashara ambao wanataka kutumia ardhi ya misitu kujenga nyumba. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wana maoni haya haya, kama alivyoandika mhariri wa “Müncher Merkur”:

“Pengine nchi hii hatimaye itaamka na kuchukua hatua kali dhidi ya wale waliosababisha moto huo kwa makusudi, vilevile dhidi ya wafanyabiashara hao kama ilivyodaiwa na wakosoaji wa serikali hiyo ya kihafidhina. Kwa muda mrefu mno, kuchoma moto misitu kwa azma ya kupatikana ardhi ya kujenga kilikuwa kitendo ambacho hakikulainiwa. Ikiwa serikali itashindwa kupambana na moto huo na kuuzima, basi kuangushwa kwa serikali itakuwa hatua ya mwisho wa janga hilo.”

Serikali ya Ugiriki tayari imetoa zawadi ya kitita cha fedha kwa mtu atakayetoa habari zitakazosaidia kukamatwa watu waliosababisha moto huo kwa makusudi. Hata hivyo, mhariri wa “Tageszeitung” la mjini Berlin ameandika:

“Kwa kuwashutumu wahalifu wa kawaida kusababisha moto huo, waziri mkuu wa Ugiriki Karamanlis anatafuta suluhisho rahisi mno. Kwa upande mmoja inaonekana kama anataka kugeuza macho wasione vile serikali ilivyoshindwa kuzuia moto huo kuripuka. Kwa upande mwingine hajajibu suali kwa nini serikali yake haikuuzima moto huo na kuzuia mwingine katika siku za nyuma unayosababishwa ili kupatikana ardhi ya kujengea. Iwapo wafanyabiashara hao bado wana matumaini ya kupata ardhi hiyo kwa ajili ya kujenga badala ya kupanda miti mipya, basi hilo ni kosa la idara husika za serikali.”

Ni gazeti la “Tageszeitung”. Mhariri wa “Nürnberger Zeitung” anailinganisha hali nchini Ugiriki na ile katika nchi nyingine Kusini mwa Ulaya. Ameandika:

“Ni siri iliyo wazi kuwa majanga mengi ya moto yanayotokea katika nchi kama Ugiriki, Italy, Spain au Kusini mwa Ufaransa yanasababishwa kwa kimakusudi. Wafanyibiashara wa ardhi wanaanzisha moto wakijua kuwa maafisa wa serikali ambao hawajui la kufanya au waliopewa rushwa wataruhusu ardhi iliyotokana na moto itumike kujengewa. Inaonekana kama serikali za nchi husika hazina uwezo kuyazuia haya. Kote inajulikana kwamba wanasiasa wa mikoa na wafanyibiashara wa sekta ya ujenzi huwa wana mahusiano ya karibu.”

Na hatimaye katika udondozi huu wa leo wa magazeti ni gazeti la “Financial Times Deutschland” ambalo linazingatia ziara ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani huko China na maonyo yake kwa Wachina kutoiga teknolojia ya Kijerumani. Ufuatao ni uchambuzi wa gazeti hili:

“Maonyo ya Bi Merkel dhidi ya Wachina ni sawa, lakini hayatasaidia chochote bila ya nchi za Magharibi kuwa na msimamo wa pamoja. Mfano ni shirika la biashara duniani ambalo badala ya kuionyesha China sheria za biashara ni zipi, nchi za Ulaya zinapigana juu ya kuuza bidhaa zao kwenye soko kubwa la China. Kwenye ziara yake, Kansela Merkel, kama kawaida, anasindikizwa na mameneja wanaotaka kutia saini mikataba ya biashara. Lakini makampuni ya nchi za Magharibi hayatafanikiwa kuzuia China kuiga teknolojia zake pale ambapo yanashindana tu badala ya kushirikiana.”

 • Tarehe 27.08.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHS1
 • Tarehe 27.08.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHS1