Moon Jae-in atarajiwa kutangazwa rais mteule wa Korea Kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Moon Jae-in atarajiwa kutangazwa rais mteule wa Korea Kusini

Tayari washindani wawili wakuu dhidi ya Moon katika uchaguzi huo, Hong Joon-pyo, mhafidhina na Ahn Cheol-soo wa siasa za mrengo wa kati wamekubali kushindwa hali inayomwachia Moon Jae-in ushindi wa moja kwa moja.

Mgombea urais nchini Korea Kusini anayefuata nadhari za kiliberali Moon Jae-in, anatarajiwa kutangazwa rais mteule wa Korea Kusini baada ya uchaguzi wa rais nchini humo. Washindani wawili wametangaza kukubali kushindwa huku matokeo ya awali yakionesha kuwa Moon amepata ushindi mkubwa.

Tayari washindani wawili wakuu dhidi ya Moon katika uchaguzi huo, Hong Joon-pyo, mhafidhina na Ahn Cheol-soo wa siasa za mrengo wa kati wamekubali kushindwa, hatua inayompa ushindi wa moja kwa moja Moon Jae-in kuwa rais, na kuhitmisha utawala wa mwongo mzima wa chama cha wahafidhina na kujitenga na sera ya sasa ya makabiliano na Korea kaskazini kuhusiana na mipango yake ya silaha za nyuklia na makombora.

Wapiga kura wengi wajitokeza

Wapiga kura Korea Kusini

Wapiga kura Korea Kusini

Uchunguzi wa maoni ya wapigakura uliofanywa kwa pamoja leo kwa niaba ya vituo vitatu vya runinga ulionyesha kuwa Moon mwenye umri wa miaka 64 alitazamiwa kupata ushindi wa asilimia 41.4 za kura huku mshindani wake wa karibu akipata asilimia 23.3 za kura

Akitangazwa mshindi rasmi, basi Moon Jae-in anayetokea chama cha upinzani cha Democratic atachukua nafasi ya Park Geun-hye, aliyeondolewa madaraka mwezi Disemba kupitia kura ya kutokuwa na imani naye kufuatia madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka. Madai ambayo mahakama ya kikatiba iliathibitisha mwezi Machi hivyo akawa rais wa kwanza wa Korea Kusini kuondolewa madarakani kwa njia hiyo.

Moon ambaye zamani alikuwa mwanajeshi, mwanaharakati wa demokrasia na wakili wa haki za binadamu, anapendelea mazungumzo na Korea ya Kaskazini kama njia ya kutuliza taharuki inayoendelea kutanda dhidi ya Korea Kaskazini kujiimarisha kisilaha.

Wapiga kura wengi wajitokeza

Rais aliyeondolewa madarakani Park Geun-Hye

Rais aliyeondolewa madarakani Park Geun-Hye

Kadhalika anataka kufanya mageuzi ya kuimarisha ufanisi wa kampuni kama za Samsung na Hyundai na kubuni nafasi zaidi ya ajira kwa vijana. Mara baada ya kupiga kura, Moon alisema Wakorea Kusini wanahitaji mabadliko. "Ninahisi kuwa si mimi pekee wala chama changu pekee, bali raia pia wamekuwa na shauku ya mabadiliko ya serikali. Ninawashukuru raia kwa kuwa nasi."

Rais mpya atakabiliwa na changamoto ya kukabili mzozo na China ambayo imeghadhabishwa na uamuzi wa Korea Kusini kutumia mfumo wa Marekani ujulikanao kama THAAD wa kujikinga dhidi ya makombora, hali ambayo China inatizama kama kitisho.

Awali, tume ya kitaifa inayosimamia uchaguzi nchini Korea Kusini ilisema idadi kubwa ya wapiga kura ijitokeza kushiriki uchaguzi huo.

Rais mpya ataapishwa kesho, kisha atatarajiwa kumteua Waziri Mkuu haraka iwezekanavyo ili aidhinishwe na bunge.

 

Mwandishi: John Juma /RTRE/DPAE/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com