1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa nchi za Sahel na wafadhili unafanyika Brussels.

23 Februari 2018

Mkutano utakaoangazia vita dhidi ya ugaidi kwenye eneo la Sahel linaloundwa na nchi tano za kiafrika unafanyika hii leo (23.02.1018) kwa kuwakutanisha wakuu wa nchi hizo pamoja na wafadhili mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/2tBuY
Gipfeltreffen in Bamako Mali
Mkutano wa G5 na wafadhili uliofanyika 2017Picha: Reuters/L. Gnago

Mkutano utakaoangazia vita dhidi ya ugaidi kwenye eneo la Sahel linaloundwa na nchi tano za kiafrika unafanyika hii leo kwa kuwakutanisha wakuu wa nchi hizo pamoja na wafadhili mjini Brussels. Kwa kipindi cha masaa matatu pekee mkutano huo una lengo la kujadili misaada ya wafadhili na changamoto za kiusalama zinazotokana na vitendo vya kigaidi kwenye eneo hilo.

Tangu mwaka 2012 eneo la Sahel limekabiliwa na machafuko huku sehemu kubwa ya taifa la Mali ikikaliwa na makundi ya waislamu wenye itikadi kali na wanajeshi wa Ufaransa wamekuwa wakikabiliana nao. Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamekuwepo kwenye eneo hilo tangu mwaka 2013 lakini makundi ya waasi yameendelea kufanya mashambulizi. Wakati huo huo waasi hao wameendelea kusambaa kwenye nchi jirani za Burkina Faso na Niger.

Akizungumza mwishoni mwa juma lililopita kwenye mkutano wa kimataifa wa usalama uliofanyika mjini Munich kusini mwa Ujerumani, Rais wa Burkina Faso, Roch Mac Christian Kabore, alisema kuwepo kwa maeneo makubwa ambayo hayadhibitiwi kikamilifu na serikali, kulinda mipaka ambayo inatoa mwanya kwa watu kuvuka bila kutambuliwa, vinarahisisha kuwepo kwa makundi ya kigaidi na kujipenyeza kwa makundi ya uhalifu na walanguzi wa biashara haramu ya binadamu.

Wahalifu watumia mianya ya mipaka kutimiza azma yao

Magenge ya kimataifa hulitumia eneo hilo kwa biashara haramu ya ulanguzi wa dawa za kulevya kuelekea barani Ulaya. Kwa kutumia wanajeshi 5000 muungano wa kikanda unaozijumuisha nchi tano G5, zikiwemo Burkina Faso, Mali, Mauritania na Chad, unataka kuzuia biashahara hiyo, wazo lilioanzishwa mwaka 2015. Kikosi hicho kinatarajiwa kuwa tayari kuanza kazi kufikia katikati ya mwaka huu.

Hili lakini huenda likawa gumu, kwani nchi wanachama wa G5 zimefaulu kupata makao makuu ya pamoja na mfumo wa kamandi ya pamoja, lakini bado kunakosekana vifaa na mafunzo.

Sahel Konflikt - Malische Armee
Vikosi vya jeshi la Mali eneo la SahelPicha: Getty Images/AFP/D. Benoit

Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki ambaye ni raia wa Chad, moja ya nchi zilizo kwenye kundi la G5, anatambua umuhimu wa nchi wafadhili kutoa msaada wa kupambana na yale yanayoendelea kwenye nchi hizo.

"Licha ya juhudi zilizochukuliwa na nchi za ukanda huo, kiwango cha uhalifu wa makundi hayo kinazidi uwezo wa  eneo na pia wa bara. Inahusu magaidi, usafirishaji haramu unaovuka mipaka. Inahusu wanajihadi. Yote hayo ni tishio kwa amani na usalama duniani, kunahitajika juhudi za pamoja kupambana na vitisho hivyo."  Alisema Mwenyekiti huyo wa kamisheni ya umoja wa Afrika.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani aliwahi kuzungumzia hali ya usalama wa ukanda wa Sahel kwenye mkutano na viongozi wa mataifa ya Sahel mwezi Desemba mwaka uliopita, akisema Ulaya inalishughulikia suala la Sahel kwa mwendo wa kinyonga na kwamba ugaidi unaofanywa na makundi ya kigaidi yenye itikadi kali ya kiislamu unaenea. Merkel pia alisema si jambo la busara kuendelea kusubiri, na kusisitiza kwamba ni lazima kuanza haraka kuongoza vita hivyo.

Wakosoaji wanasema hawaamini kama nchi za kundi la G5 zinaweza kutoa upinzani wowote kwa makundi ya kigaidi bila msaada utakaoleta maendeleo. Makundi hayo yalipoiteka sehemu kubwa ya Mali mwaka 2012, jeshi lilishindwa kuyadhibiti. Hali ya usalama ya eneo la Sahel inaendelea kuwa mbaya ambapo wiki kadhaa zilizopita watu 36 waliuawa baada ya gari lao kulipuliwa na mabomu ya kutegwa ardhini.

Mwandishi: Pelz, Daniel (HA Afrika)
Tafsiri: Angela Mdungu
Mhariri: Josephat Charo