Misri ina matumaini kuwa Israel, Hamas watafikia makubaliano
29 Aprili 2024Kauli hiyo ya Misri imetolewa leo na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Sameh Shoukry, kando ya mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi la Dunia unaoendelea mjini Riyadh nchini Saudi Arabia. Shoukry amesema anatumai pendekezo hilolitazingatia misimamo ya pande zote mbili na kwamba wanasubiri uamuzi wa mwisho:
"Kuna pendekezo ambalo lipo mezani, na linapaswa kutathminiwa na kukubaliwa na pande zote mbili, lakini kwa hakika lengo kuu ni usitishaji wa kudumu wa mapigano na kushughulikia hali ya kibinadamu."
Hata hivyo, Misri imetaja kushtushwa na mpango wa operesheni ya kijeshi ya ardhini ya Israel huko Rafah wanakoishi zaidi ya watu milioni moja waliokimbia mapigano katika maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza. Watu wasiopungua 30 wameripotiwa kuuawa huko Rafah kufuatia mashambulizi mapya ya jeshi la Israel.
Katika miezi ya hivi karibuni, mataifa ya Misri, Qatar na Marekani yamekuwa yakizidisha juhudi za kuyafufua mazungumzo yaliyokwama kati ya Israel na kundi la Hamas ili hatimaye kufikiwe makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiwa kwa mateka.
Soma pia: Hamas inatathmini pendekezo jipya la Israel la kusitisha mapigano
Kundi la Hamas ambalo limeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya magharibi kuwa kundi la kigaidi lilisema siku ya Jumamosi kwamba limepokea na kuanza kutathmini pendekezo jipya la Israel la kusitisha mapigano. Ujumbe wa kundi hilo umewasili hii leo mjini Cairo ili kuendeleza mazungumzo hayo.
Kwa upande mwingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema kumeshuhudia maendeleo kidogo katika hali ya kibinadamu huko Gaza, lakini akaonya kuwa misaada inayowasilishwa huko bado haitoshi na akaapa kuwashinikiza viongozi wa Israel baadaye wiki hii ili kuchukua hatua zaidi.
Msimamo wa Marekani kuhusu mzozo huu
Akihutubia mkutano wa pamoja kati ya Marekani na mataifa sita wanachama wa Baraza la ushirikiano wa Ghuba, Blinken ameiahidi Saudi Arabia kuwa Washington iko tayari kuidhinisha kifurushi cha mpango wa usalama ikiwa tu itarekebisha mahusiano yake na Israel.
Serikali mjini Riyadh kama sehemu ya makubaliano hayo, inatarajiwa kusisitiza juu ya suala la uwepo wa taifa huru la Palestina na vile vile dhamana ya usalama kutoka Marekani.
Soma pia: Netanyahu aafiki kuanzishwa duru mpya ya mazungumzo ya usitishwaji mapigano Gaza
Aidha Blinken amesema ana matumaini kuwa Hamas itakubali pendekezo alilolitaja kuwa lenye "ukarimu wa ajabu" la kusitisha mapigano huko Gaza kwa muda wa siku 40, sambamba na kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel.
Hayo yakiarifiwa, Israel imeelezea hii leo wasiwasi wake kuhusu taarifa kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC imekuwa katika maandalizi ya kutoa waranti wa kukamatwa kwa baadhi ya maafisa wa serikali ya Tel-Aviv kwa tuhuma zinazohusiana na mienendo yao katika vita vyake dhidi ya kundi la Hamas.
(Vyanzo: Mashirika)