Miaka 100 ya kuzaliwa Mandela | Matukio ya Afrika | DW | 18.07.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Miaka 100 ya kuzaliwa Mandela

Afrika Kusini na ulimwengu kwa jumla inaadhimisha miaka 100 tangu alipozaliwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo ambaye aliongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi Nelson Mandela.

Kutakuwa na kongamano ambalo Rais wa zamani wa Marekani Barrack Obama atalihutubia na pia kufanyika matembezi yatakayoongozwa na mjane wa Mandela miongoni mwa mambo mengine. 

Siku ya kuzaliwa Mandela mnamo Julai 18 inaadhimishwa kila mwaka kote duniani ikifahamika kama "Siku ya Mandela”, na wakfu wa Nelson Mandela ukawataka watu "kuchukua hatua ya kuhimiza mabadiliko” kwa kumuenzi kiongozi huyo katika mwaka wake wa 100 tangu alipozaliwa.

Obama, akizungumza jana mbele ya watu 15,000 katika uwanja wa michezo mjini Johannesburg, alitoa hotuba yenye hisia nyingi akikumbusha kuhusu "wimbi la matumaini ambalo liliipiga mioyo ya watu kote duniani” wakati Mandela alipoachiliwa huru kutoka gerezani mwaka wa 1990.

Südafrika Obamas Besuch

Obama awataka vijana kupigania demokrasia

Mandela, ambaye alifariki mwaka wa 2013, anabaki kuwa shujaa wa ulimwengu kwa vita vyake vya muda mrefu dhidi ya utawala wa wazungu walio wachache na kwa ujumbe wake wa Amani na maridhiano wakati alipoachiwa huru baada ya kuishi miaka 27 gerezani

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, mwanafunzi wa Mandela ambaye aliingia madarakani mwaka huu, amesema ataadhimisha siku hii ya Mandela 100 kwa kutoa nusu ya mshahara wake kwa shirika la hisani na akatoa wito kwa wengine kufanya hivyo. Ramaphosa yuko katika eneo la Mvezo, mkoa wa Cape Mashariki, alikozaliwa Mandela, akiongoza sherehe hizo ikiwa ni pamoja na kuzindua kliniki, sherehe ya kupanda miti na kutoa blanketi kwa wazee.

Graca Machel, mjane wa Mandela, ataongoza matembezi mafupi kuendeleza sifa ya Mandela, huku pia siku hii ya miaka 100 ikiadhimishwa kwa uzinduzi wa kitabu kipya cha barua zake zilizoandikwa akiwa jela na pia kutolewa sarafu ya fedha.

Obama atawahutubia vijana 200 waliochaguliwa kutoka kote Afrika kuhudhuria kozi ya siku tano mjini Johannesburg kuhusu masuala ya uongozi.

Mandela alifungwa jela chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi mwaka wa 1962 na akaachiwa huru mwaka wa 1990, wakati alipokiongoza chama cha African National Congress kupata ushindi katika uchaguzi wa kwanza wa jamii zote mwaka wa 1994. Alihudumu kwa muhula mmoja kama rais kabla ya kujiuzulu mwaka wa 1999.

Mwandishi: Bruce Amani/AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga