Merkel kuanza ziara leo Kenya
11 Julai 2011Miongoni mwa maswala mbayo kiongozi huyo wa ujerumani anarajiwa kuyagusia ni amani katika eneo la Mashariki na Pembe ya Afrika hasa ukosefu wa usalama nchini Somalia.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi, Balozi wa Ujerumani nchini Kenya, Bi Margit Helwig-Boette amesema “Tuna lengo la pamoja la kupambana na uharamia ambapo Kenya ni mshirika muhimu katika lengo hili kwa hivyo ziara ya Kansela Merkel imejumuisha malengo ya kisiasa na kiuchumi yanayohusu eneo hili”.
Ziara ya Kansela Merkel inafanyika wakati ambapo Kenya iko katika harakati za kutekeleza mageuzi ya kisiasa na mfumo mpya wa uongozi ambapo Ujerumani imechangia kwa kiasi kikubwa mageuzi hayo ikiwemo katiba mpya.
Balozi wa ujerumani nchini Kenya Margit Helwig-Boette akifafanua juu ya ziara ya Merkel amesema, hii ni ziara ya kwanza ya Kansela Merkel nchini Kenya na nina hakika kwamba atatumia nafasi hii ya mazungumzo ya moja kwa moja kati yake na Waziri Mkuu na Rais kupata msimamo kamili wa serikali ya Kenya katika utekelezaji agenda ya mageuzi na hasa utekelezaji wa katiba.
Balozi Margit amesisitiza wito uliotolewa hivi karibuni na Tume ya Umoja wa Ulaya kwamba viongozi wa Kenya wanapaswa kushirikiana kuhakikisha katiba mpya inatekelezwa ili kuandaa mazingira bora ya kisiasa kabla uchaguzi mkuu mwaka ujao.
Ni kutokana na swala hilo ambapo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amepangiwa kufanya mashauri na spika wa bunge Keneth Merende hapo kesho.
Ziara ya Kansela huyo wa Ujerumani nchini Kenya bila shaka itatoa fursa nzuri ya kuimarisha Biashara kati ya nchi hizo mbili.
Uhusiano wa Kenya na Ujerumani ulianza mwaka 1950 na tangu wakati huo hadi sasa Kenya imepokea msaada kutoka serikali ya Ujerumani wa jumla ya Euro Bilioni 1.4 . Mwaka uliopita pekee, serikali ya ujerumani iliipa Kenya msaada wa Euro milioni 140 fedha ambazo zilipangiwa kutumika katika sekta ya kilimo na Nishati.
Baada ya kukutana na viongozi wa serikali ya Kenya Kansela Angela Merkel atazuru Taasisi ya Kimataifa ya utafiti wa Mifugo iliyoko mjini Nairobi na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP kabla ya kuondoka kuelekea nchini Angola hapo kesho jioni.
Mwandishi Alfred Kiti
Mhariri Yusuf Saumu◄