1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aapa kushirikiana na SPD

Mohammed Khelef
4 Machi 2018

Kansela Angela Merkel ameapa kushirikiana na chama cha Social Democrat kwa ajili ya maslahi ya Ujerumani, baada ya chama hicho cha mrengo wa kati kushoto kupiga kura kuridhia kuunda serikali ya muungano.

https://p.dw.com/p/2tfX3
Angela Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Zaidi ya wanachama 460,000 wa SPD walipiga kura kuamua endapo chama chao kijiunge na muungano wa kihafidhina unaoongozwa na Kansela Merkel ama la, na uamuzi wao unatajwa kuwa kikomo cha mkwamo wa kisiasa ulioikumba Ujerumani tangu mwezi Septemba 2017, kufuatia uchaguzi ambao haukutoa mshindi wa moja kwa moja kuweza kuunda serikali.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo mkongwe anaingia kwenye muhula wake wa nne - na yumkini wa mwisho - akiwa na uwezo mdogo zaidi ya ule wa awali kwenye serikali ya mseto.

"Kansela Merkel, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 12 sasa, atapaswa kulipia gharama ya kura hii ya leo kwa kuichukuwa SPD kwenye muungano usiokuwa na mapenzi baina yao," wanasema baadhi ya wachambuzi. 

Akiipongeza SPD kwa uamuzi kile alichokiita "matokeo ya wazi", Kansela Merkel alitumia mtandao wa Twitter wa chama chake cha CDU kusema kwamba anatazamia kushirikiana nao "kwa maslahi mapana ya nchi."

SPD yamaliza ikiwa imejeruhiwa

Mkuu wa tawi la vijana la SPD, Kevin Kühnert, ambaye aliongoza kampeni ya kukataa chama chake kujiunga na CDU/CSU.
Mkuu wa tawi la vijana la SPD, Kevin Kühnert, ambaye aliongoza kampeni ya kukataa chama chake kujiunga na CDU/CSU.Picha: picture-alliance/Zumapress/S. Babbar

Awali SPD iliwahi kuondoa kabisa uwezekano wa kuingia kwenye serikali ya mseto, kufuatia matokeo mabaya waliyoyapata kwenye uchaguzi mkuu, lakini baada ya jitihada za Merkel kuunda serikali na vyama vyengine vidogo kushindwa, chama hicho kilibadilisha msimamo wake.

Hata hivyo, kutokana na hofu ya kupoteza zaidi imani ya wanachama wake, SPD iliwaahidi wanachama hao kwamba wangeliamua wenyewe makubaliano yoyote ya serikali ya mseto iajyo.

"Sasa tuna uhakika. SPD itajiunga na serikali ijayo," alisema mwenyekiti wa mpito wa SPD, Olaf Scholz, aliyeongeza pia kwamba chama chake kinapanga kupeleka mawaziri wengine sita kwenye baraza la mawaziri - watatu wakiwa wanaume na watatu wanawake.

Ulaya yaipongeza SPD

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa (kushoto) amempongeza Kansela Angela Merkel (kulia) na chama cha SPD.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa (kushoto) amempongeza Kansela Angela Merkel (kulia) na chama cha SPD.Picha: picture-alliance/abaca/D. Aydemir

Washirika wa Ujerumani barani Ulaya walisubiri kwa muda mrefu kwa taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi miongoni mwa wanachama wa Umoja wa Ulaya, ambapo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameuita uamuzi wa SPD kuwa ni "habari njema kwa Ulaya."

"Ufaransa na Ujerumani zitashirikiana kuanzia wiki chache zijazo kukuza mipango ya kuupeleka mbele mradi wa Ulaya," ilisema ofisi ya Macron.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Frans Timmermans, aliandika kwenye Twitter: "GroGo! Kwa mshikamano wa Ujerumani na Ulaya!" GroKo, na sio GroGO, ni kifupisho cha Grand Koalition kwa Kijerumani, yaani muungano mkuu, kuashiria serikali ya mseto inayoundwa na vyama vikuu vya SPD, CDU na CSU.

Kufuatia uamuzi huu wa SPD kuingia serikalini, Kansela Merkel anatazamiwa kutangaza baraza lake la mawaziri katikati ya Machi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Lilian Mtono