Mazungumzo ya amani ya Ukraine yameanza | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.12.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya amani ya Ukraine yameanza

Wawakilishi wa serikali ya Ukraine na waasi wanaoiunga mkono Urusi, wameanza awamu nyingine ya mazungumzo muhimu yenye lengo la kumaliza mzozo wa Ukraine, miezi mitatu baada ya kukubaliana kusitisha mapigano.

Rais Poroshenko akiwa na Rais Putin

Rais Poroshenko akiwa na Rais Putin

Mazungumzo hayo ya amani ya pande tatu yanayowakutanisha wawakilishi kutoka serikali ya Ukraine na upande wa waasi pamoja na wapatanishi kutoka Urusi na Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya-OSCE, yanafanyika leo kwenye mji mkuu wa Belarus, Minsk, na huenda yakafungua njia ya mkutano wa pili uliopangwa kufanyika siku ya Ijumaa.

Mazungumzo hayo yanajadili namna ya kuondoa silaha nzito za kijeshi kutoka mashariki mwa Ukraine na kubadilishana wafungwa wa kivita na yatasaidia kuimarisha makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Septemba. Shirika la habari la Urusi, Tass, limeripoti kuwa waasi wanataka Ukraine iondoe kizuizi cha kiuchumi katika mikoa inayodhibitiwa na waasi.

Balozi wa Urusi nchini Ukraine, Mikhail Zubarov ambaye pia ni mjumbe wa Urusi kwenye mazungumzo hayo, anayeegemea upande wa waasi, amesema masuala ya kiuchumi ni moja ya ajenda nne muhimu zitakazojadiliwa leo.

Kiongozi wa waasi wa Luhansk, Igor Plotnitsky

Kiongozi wa waasi wa Luhansk, Igor Plotnitsky

Lakini mwakilishi wa OSCE kutoka Ukraine ambaye pia atahudhuria mkutano huo, Heidi Tagliavini, amesema pande hizo zitajadili namna ya kufikisha misaada ya kibinaadamu.

Kiongozi wa waasi wa Luhansk ambaye ni mwakilishi wa waasi, Igor Plotnitsky, amesema hadi sasa haoni iwapo mazungumzo hayo yatazaa matunda yoyote yale na wala hana matumaini kama wataweza kufikia makubaliano.

Hatua imefikiwa baada ya mazungumzo ya simu ya viongozi

Nchi hizo zilikubaliana kukutana mjini Minsk, baada ya kufanyika mazungumzo ya simu siku ya Jumatatu kati ya Rais Vladmir Putin wa Urusi na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Rais Petro Poroshenko wa Ukraine.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 4,600 wameuawa na wengine milioni moja nukta moja hawana makaazi, tangu yalipozuka mapigano mwezi Aprili mwaka huu.

Mvutano kuhusu mzozo wa Ukraine ulizidi kuongezeka hapo jana baada ya bunge la Ukraine kupiga kura kwa kauli moja kuunga mkono hatua ya kuachana na hadhi ya nchi hiyo kutoegemea upande wowote, hatua inayoelekeza juhudi za nchi hiyo kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Jengo lenye ofisi za OSCE, Minsk

Jengo lenye ofisi za OSCE, Minsk

Hatua hiyo iliikasirisha vibaya Urusi, ambayo ilisema haileti tija na badala yake inazidisha mvutano mashariki mwa Ukraine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema hatua hiyo inazidisha mapambano na ina chochea zaidi hali ya mashariki kuwa mbaya.

Uhusiano kati ya Urusi na Ukraine umekuwa mbaya tangu Crimea ilivyojitenga na Ukraine na kujiunga na Urusi mwezi Machi mwaka huu, na baadaye kuzuka kwa waasi wa mashariki wanaoiunga mkono Urusi. Hata hivyo, Urusi imekuwa ikikanusha kuhusika na mzozo wa mashariki mwa Ukraine, ikisema kuwa huo ni mzozo wa ndani wa Ukraine.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com