Mawaziri wa nishati wa Marekani na Ulaya wakutana Ugiriki
7 Novemba 2025
Mawaziri wa nishati kutoka Marekani na nchi za Ulaya wamefanya mazungumzo jana Alhamisi nchini Ugiriki kuhusu jinsi ya kutumia mtandao mpya wa mabomba ya kikanda ulioboreshwa ili kuisambazia vyema nishati Ukraine iliyoharibiwa na vita huku utawala wa Trump ukitaka kuongeza zaidi mauzo ya nje ya gesi kwenda Ulaya.
Maafisa wakuu wa Marekani wamewasihi washirika wa Ulaya jana Alhamisi kuharakisha uondoaji wa gesi ya Urusi kwa kupanua mitandao ya mabomba ya kikanda na kuongeza uagizaji wa gesi asilia iliyoyeyushwa ya Marekani kote Ulaya.
Waziri wa nishati wa Marekani Chris Wright na waziri wa mambo ya ndani Doug Burgum walijiunga na maafisa zaidi ya 80 wa Marekani, mawaziri wa nishati wa Umoja wa Ulaya na watendaji wakuu wa makampuni ya gesi asilia iliyoyeyushwa kwa mazungumzo nchini Ugiriki yaliyoandaliwa na Baraza la Atlantiki, shirika la kutoa ushauri wa kitaalamu lenye makao yake makuu mjini Washington.
"Marekani pekee ndiyo inayoweza kuifuta nafasi ya gesi yote ya Urusi barani Ulaya kwa kile tunachokijenga," alisema Burgum, akiashiria nia kali ya Marekani ya kujaza pengo lililoachwa na kupunguzwa kwa usambazaji wa gesi ya Urusi.
Shinikizo hilo linakuja huku Rais Donald Trump akiendelea kutumia nafasi ya Marekani kama muuzaji nje mkuu wa gesi asili iliyoyeshwa duniani, akiunganisha usambazaji wa nishati na uhusiano wa kibiashara na Ulaya na juhudi za kukomesha vita nchini Ukraine.
Marekani yakosoa sheria za hali ya hewa za Umoja wa Mataifa
Burgum pia alizilenga na kuzikosoa kanuni za hali ya hewa za Ulaya, akidai zinaweza kusimamisha ushirikiano katika masuala ya nishati. lisema hakuna kipindi cha mpito cha matumizi ya nishati, badli kuna nyongeza ya nishati tu, akiongeza kwamba hali ya udhibiti barani Ulaya inahatarisha kuizuia kanda hiyo kutokana na wimbi lijalo la uvumbuzi wa nishati na maendeleo ya akili mnemba inayotamani nishati.
Kwa kuwa Ulaya tayari ndiyo soko kubwa zaidi la gesi asili iliyoyeshwa ya Marekani, mwelekeo umeelekezwa kwenye kinachojulikana kama Ukanda wa Wima - njia mpya ya usafirishaji gesi kutokea eneo la kaskazini kuelekea kusini inayounganisha Ugiriki na Bulgaria, Romania na Ukraine. Vituo vya usafirishaji nje karibu na mji wa Athens na kaskazini mwa Ugiriki vitakuwa na jukumu muhimu.
Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis alisema Jumatano jioni. "Ugiriki imebarikiwa na eneo la kipekee sana la kijiografia, na sisi ndio kiingilio cha asili cha gesi asilia iliyoyeyushwa ya Marekani kuingia Ulaya,"
Ulaya inajitahidi kuboresha mabomba
Maafisa wa Marekani na Ulaya walisema ukanda huo unaweza kuwa muhimu katika kusaidia Ukraine iliyokumbwa na vita kukabiliana na mashambulizi yasiyokoma ya Urusi dhidi ya miundombinu yake ya nishati. Kufuatia uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo 2022, wanachama wa Umoja wa Ulaya walijitahidi kurekebisha mitandao ya mabomba ili kuchukua nafasi ya mauzo ya nje ya Urusi na gesi asili iliyoyeshwa inayotolewa na Marekani na wauzaji wengine wakuu.
Wright, waziri wa nishati wa Marekani, alikaribisha mipango ya Halmashauri ya Ulaya ya kuondoa usambazaji wote wa gesi wa Urusi kwa Umoja wa Ulaya katika kipindi cha miaka miwili ijayo, akisema "itazinyima nyenzo za vita za Urusi na kujenga uhusiano unaokua wa siku zijazo" kati ya mataifa ya Ulaya na Marekani. Wright aidha alisema "Wana mabomba matano yanayokuja Ulaya na bomba moja linalokwenda China," akimaanisha Urusi.
Ukraine inakabiliwa na majira ya baridi kali
Akizungumza na shirika la habari la The Associated Press kando ya mkutano wa mjini Athens, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kibinafsi ambayo ni mzalishaji mkubwa zaidi wa nishati nchini Ukraine DTEK, Maxim Timchenko, alionya kuhusu changamoto kubwa. Timchenko aliuelezea mkutano wa Athens kama "muhimu sana," na akazitaka nchi za Ulaya na Marekani kusaidia kusambaza gesi na vifaa vya ziada ili kutengeneza gridi ya umeme ya Ukraine.
"Majira haya ya baridi yanayokuja labda yatakuwa majira ya baridi magumu zaidi tangu uvamizi kamili," Timchenko alisema. "Tunahitaji msaada. Tunahitaji msaada katika usambazaji wa gesi, tunahitaji msaada katika usambazaji kwa ajili ya uzalishaji wetu wa umeme." DTEK ilizindua matumizi ya Ukraine ya "Ukanda maalumu wa usafirishaji gesi kutoka kaskazini hadi kusini" mapema mwaka huu, pamoja na usafirishaji wa gesi asili iliyoyeshwa kutoka Louisiana nchini Marekani hadi Ugiriki.
Kando na hayo, washirika wa Marekani na Ugiriki Alhamisi walitangaza uwekezaji zaidi katika eneo la mashariki mwa Mediterania. Makampuni ya Exxon Mobil, pamoja na Helleniq Energy na kampuni ya Energean ya Ugiriki, zilithibitisha mipango mipya ya utafutaji wa mafuta na gesi katika Bahari ya Ionian, sehemu ya mkakati mpana wa kampuni ya Marekani wa kutanua uwezo wa nishati katika eneo hilo.