Mawaziri wa fedha wa kanda ya Euro wakutana Brussels | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.02.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mawaziri wa fedha wa kanda ya Euro wakutana Brussels

Serikali ya Ujerumani imeregeza kamba kuelekea pendekezo la Ugiriki la kurefushiwa muda wa mpango wa msaada ,ikisema ingawa pendekezo hilo linahitaji marekebisho,lakini linafungua njia ya kuendelezwa mjadiliano

default

Nembo ya mgogoro wa fedha wa Ugiriki

Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Wolfgang Schäuble aliwashangaza washirika wake wa Ulaya na mawaziri wenzake serikalini alipoitaja risala ya waziri mwenzake wa fedha wa Ugiriki kuwa ni mbinu za kudai misaada zaidi bila ya kukubali kufanya mageuzi na kufunga mkaja.

Lakini wakati mkutano muhimu wa mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro ukikurubia kuanza mjini Brussels ,kansela Angela Merkel,kupitia msemaji wake,amesawazisha mambo akimsifu wakati huo huo waziri wake wa fedha na kusema serikali yake ina msimamo mmoja.

"Risala ya waziri wa fedha wa Ugiriki inadhihirisha kwamba Ugiriki ingali bado inapendelea kupata msaada wa Umoja wa Ulaya" amesema msemaji wa kansela Merkel,bibi Christiane Wirtz na kuongeza tunanuku:"Risala hii ni dalili njema inayoturuhusu tuedelee kujadiliana."Mwisho wa kumnukuu.

Ameongeza kusema mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro wanaokutana jioni hii mjini Brussels wataendelea kujadiliana kwa msingi wa risala hiyo-akielezea wakati huo huo matumaini ya kuyaona mazungumzo hayo yakipelekea kufikiwa makubaliano pamoja na Ugiriki.

Alexis Tsipras ahimiza uamuzi wa kishitoria uchukuliwe

Yanis Varoufakis

Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis (kulia) na mwenyeki wa kundi la nchi za Umoja wa ulaya zinazotmia sarafu ya Euro Jeroen Dijsselbloem

Kwa upande wake waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras ameliamia shirika la habari la Uengereza Reuters "ana hakika maombi ya serikali yake ya kurefushwa kwa miezi sita muda wa mpango wa misaada yatakubaliwa.Ametoa wito wa kupitishwa kile alichokiita "uamuzi wa kihistoria kwa mustakbal wa Ulaya" .

Alexis Tsipras amesema nchi yake imefanya kila liwezekanalo kufikia ufumbuzi kwa manufaa ya pande zote na kwa misingi ya kuheshimu mwongozo wa sheria za Umoja wa Ulaya na pia matokeo ya uchaguzi ya nchi wanachama.

Der Spiegel yaashiria uwezekano wa kujitoa Ugiriki na kanda ya Euro

Geldautomaten vor der Griechischen Nationalbank

Milolongo ya wagiriki wakipiga foleni katika vituo vya kutoa fedha

Taarifa hiyo ya waziri mkuu wa Ugiriki imetolewa muda mfupi baada ya jarida la Ujerumani Der Spiegel kuripoti benki kuu ya Ulaya inajiandaa kukabiliana na uwezekano wa kujitoa Ugiriki na kanda ya Euro.Benki kuu ya Ulaya haijasema chochote kuhusu ripoti hiyo.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa/

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com