Matokeo ya urais Zanzibar bado hayajakamilika kutangazwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Matokeo ya urais Zanzibar bado hayajakamilika kutangazwa

Licha ya uchache wa wapiga kura inapolinganishwa na Tanzania Bara, matokeo ya kura za urais visiwani Zanzibar hayajakamilishwa kutangazwa hadi sasa na kumeanza kuzua mshawasha miongoni mwa wanasiasa.

Tayari mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wanachi, CUF, hapo jana alisema matokeo yaliyokusanywa moja kwa moja kutoka vituo vya kupigia kura yanampa yeye ushindi, kauli ambayo imekosolewa vikali na viongozi wa Chama cha Mapinduzi, CCM, visiwani humo.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, ZEC, Jecha Salim Jecha, jana alitangaza matokeo ya kura za urais kutoka majimboni katika kituo cha kutangazia matokeo cha Tume hiyo, Bwawani, Zanzibar, ingawa kama alivyosema, matokeo hayo ni ya awali na yasiyothibitishwa. Ukosefu wa ithibati na uthabiti ndio tatizo sasa la visiwani Zanzibar. Nalo limezaa hali ya kutoaminiana na kutegana.

Mgombea urais wa CUF, Zanzibar, Seif Sharif Hamad

Mgombea urais wa CUF, Zanzibar, Seif Sharif Hamad

Kufikia jana jioni, vyama viwili vyenye ushindani mkali, CCM na CUF, vilikuwa vinaielekeza kidole ZEC, huku CUF ikiitaka Tume hiyo kutangaza matokeo halisi kama yalivyokusanywa kutoka vituoni na sio kinyume chake.

Maalim Seif Sharif Hamad, mgombea urais wa chama cha CUF, jana asubuhi alijitangazia ushindi, hali iliyofanya kauli yake ijibiwe masaa tisa baadaye na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, aliyekuwa ameambatana na Waziri Kiongozi Mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha, Spika Pandu Ameir Kificho na Waziri wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Haji Omar Kheir, mbele ya waandishi wa habari, Kisiwandui.

Lakini Naibu Katibu Mkuu wa CUF visiwani Zanzibar, Nassor Mazrui, anasema kilichofanywa hasa na mgombea wake kilikuwa ni kuonesha muelekeo halisi wa matokeo ya uchaguzi na sio kujitangazia ushindi.

CCM yatoa malalamiko

Pamoja na kulalamikia kauli hiyo ya Maalim Seif juu ya ushindi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alilalamikia pia kukamatwa kwa mtu mmoja akiwa na kura tano kwenye jimbo la Chonga, kisiwani Pemba.

Mgombea urais wa CCM, Zanzibar, Ali Mohammed Shein

Mgombea urais wa CCM, Zanzibar, Ali Mohammed Shein

Vile vile, Naibu huyo Katibu Mkuu wa CCM, alidai kuhujumiwa na baadhi ya maafisa wa ZEC katika wilaya ya Magharibi, ambao alidai waliwazuia mawakala wa chama chake kuwamo kwenye vituo vya kupigia kura.

Alipoulizwa na DW ikiwa tangazo lao hilo lilimaanisha kutokuwa na imani na matokeo yatakayotangazwa na ZEC, Waziri Kiongozi wa zamani, Shamsi Vuai Nahodha, alijibu kuwa iwapo matokeo yanatangazwa na tume ya uchaguzi, hawawezi kuwa na wasiwasi.

Kwa vyovyote vile, kitendo cha ZEC kuchukuwa zaidi ya siku mbili bila kukamilisha hesabu ya kura zisizofikia laki tano, kinazidisha hali ya wasiwasi visiwani Zanzibar, ambapo uzoefu wa chaguzi za nyuma, umejaa rangi za visa na mikasa. Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Mazrui anasema wasiwasi huo unapaswa kuondoka miongoni mwa wanasiasa kwa kuwa vyovyote matokeo yatakavyokuwa, hatimaye pande zote mbili zitaungana kwenye serikali ya umoja wa kitaifa.

Matokeo ambayo ZEC imefanikiwa kuyatangazia hadi sasa kwa nafasi ya urais ni ya majimbo 13, na DW ilishuhudia mfanano mkubwa kati ya matokeo hayo na yale yaliyochapishwa na CUF na kusambazwa kwa jumuiya ya kimataifa.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com