Mateso Libya yasababisha ongezeko la wahamiaji wanaotorokea Ulaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mateso Libya yasababisha ongezeko la wahamiaji wanaotorokea Ulaya

Shirika la kimatifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema wahamiaji kutoka Libya wanakabiliwa na mateso yanayosababisha watu wengi kuhatarisha maisha yao wakijaribu kuingia barani Ulaya.

Kwa miaka mingi taifa la Libya limekuwa kivukio cha kuingia barani Ulaya kwa maelfu ya waafrika wanaotafuta maisha bora. Wakimbizi wa Syria wanaokimbia vita nchini mwao pia wanaelekea Libya kujaribu kutumia njia hiyo kufika katika nchi za magharibi.

Mkurugenzi wa shirika la Amnesty International wa kanda ya mashariki ya kati na kaskazini mwa Afrika Philiph Luther amesema mazingira magumu yanayochochewa na ukosefu wa sheria na mapigano yanayoikumba Libya tangu kung'olewa na hatimaye kuuawa kwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi mwaka 2011, kunadhihirisha wazi ni kwa kiasi gani maisha yako hatarini katika Libya ya sasa.

Mizozo kaskazini mwa Afrika yachochea biashara haramu

Watu wanaohusika na biashara ya kuwasafirisha watu kwa njia haramu wameongeza kasi ya biashara yao kutokana na kuongezeka kwa watu wanaotoroka vita na mahangaiko na kutaka kuingia Ulaya.Kuboreka kwa hali ya hewa katika kipindi cha miezi michache iliyopita pia kumechangia kuongezeka kwa biashara haramu ya kusafirisha wakimbizi.

Maelfu ya wahamiaji kutoka Afrika katika bahari ya Mediterania

Maelfu ya wahamiaji kutoka Afrika katika bahari ya Mediterania

Luther ameutaka Umoja wa Ulaya kutuma meli zaidi za kusaidia katika shughuli za uokozi katika bahari ya Mediterania na wakati huo huo kuimarisha juhudi zao za kupambana na wafanyabishara wanaosafirisha watu kwa njia haramu.

Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya hapo jana walikutana kujadili kubadilishana taarifa za kijasusi ili kuzuia ongezeko la kuingia wahamiaji haramu barani humo hasa kutoka kaskazini mwa Afrika.

Mawaziri hao kutoka Ufaransa, Ujerumani, Poland na Uhispania wamesema kinachohitajika zaidi ni agizo la Umoja wa Mataifa ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kukabiliana na tatizo hilo.Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean Yves Le Drian amesema wameongeza juhudi za kupunguza vifo baharini

Hii leo mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini atawasilisha mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mipango ya umoja wa Ulaya kupunguza idadi ya wahamiaji wanaoingia Ulaya ambao maelfu kati yao wamekufa wakijaribu kuingia barani humo.

Maelfu wamekufa majini

Umoja wa Ulaya unalenga kulishawishi baraza hilo la usalama kuidhinisha mpango wake unaojumuisha kuharibu boti zinazoendeshwa na wafanyibiashara haramu ya kuwasafirisha wahamiaji. Zaidi ya wahamiaji 5,000 wamekufa majini katika kipindi cha miezi kumi na minane iliyopita katika bahari ya Mediterrania.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Calude Junker

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Calude Junker

Kulingana na gazeti la Uingereza la The Times, Rais wa Halamshauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker Jumatano wiki hii atawasilisha mapendekezo ya kuwepo mfumo ambao utazilazimu nchi 28 wanachama wa umoja wa Ulaya kuwahifadhi wahamiaji kwa kugawana idadi fulani kila moja.

Idadi ya wahamiaji ambao kila nchi itapewa itategemea vigezo kadha vikiwemo pato jumla la taifa, idadi ya watu,kiwango cha ukosefu wa ajira na idadi ya wahamiaji waliopewa hifadhi katika taifa.

Kulingana na sera zilizopo, nchi wanayotua kwa mara ya kwanza wahamiaji hao ndiyo inabeba mzigo wa kuhifadhi, ikimaanisha nchi kama Italia, Malta na Ugiriki zinajikuta na mzigo mkubwa wa kukidhia mahitaji ya wahamiaji.

Mwandishi: Caro Robi/afp

Mhariri: Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com