Qatar na Bahrain zarejesha uhusiano wa kidiplomasia.
13 Aprili 2023Wajumbe kutoka nchi hizo mbili za Qatar na Bahrain walikutana hapo jana Jumatano katika makao makuu ya Baraza la Ushirikiano la nchi za Ghuba GCC mjini Riyadh, Saudi Arabia. Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Ahmed bin Hassan al Hammadi alikutana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Bahrain Sheikh Abdullah bin Ahmed Al Khalifa ambapo walijadili juu ya kuusuluhisha mzozo ulioanza mwaka 2017.
Baadae wizara za mambo ya nje za nchi hizo za Qatar na Bahrain zilisema katika taarifa tofauti kwamba zinataka kuimarisha Umoja na ushirikiano wa nchi za Ghuba kulingana na Mkataba wa GCC. Mataifa sita yanayojumuisha Jumuiya hiyo ni pamoja na Bahrain, Kuwait, Qatar,Saudi Arabia, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Soma:Rais wa UAE amwambia Assad ni wakati wa Syria kurejea Uarabuni
Bahrain ni nchi ya mwisho kati ya mataifa manne ya Kiarabu ambayo yaliweka vikwazo na kuisusia Qatar mnamo mwaka wa 2017 baada ya Qatar kudaiwa kuyaunga mkono makundi ya Kiislamu yaliyoanza kutawala katika baadhi ya nchi za kiarabu zilizokumbwa na maandamano ya kupinga serikali ya mwaka 2011 maarufu "Arab Spring," ambayo baadhi ya mataifa yaliyachukulia makundi hayo kuwa ni mashirika ya kigaidi.
Hata hivyo nchi za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri ziliondoa vikwazo dhidi ya Qatar mnamo mwaka 2021 na kurejesha uhusiano na taifa jilo dogo tajiri tangu wakati huo.
Makubaliano ya Jumatano kati ya Qatar na Bahrain yamefikiwa huku kukiwa na juhudi za kikanda kwa nchi za Kiarabu zilizokua maadui kwa muda mrefu kuboresha mahusiano. Ishara ya hivi punde ni hapo jana Jumatano ambapo Saudi Arabia ilimkaribisha waziri wa mambo ya nje wa Syria. Ishara hiyo ni wazi kwamba Jumuiya ya nchi za Kiarabu iko tayari tayari kuirejesha Syria kundini baada ya kusimamisha uanachama wake kwa zaidi ya muongo mmoja.
Soma:Saudi Arabia yaukaribisha ujumbe wa Iran na Syria
Kurejeshwa kwa uhusiano kati ya mataifa ya Kiarabu kunatokea wakati ambapo zinafanyika juhudi nyingine kadhaa za kutatua mizozo ya kikanda. Imeshuhudiwa mnamo mwezi uliopita, Saudi Arabia na mpinzani wake mkuu wa kikanda, Iran, zilirejesha uhusiano wa kidiplomasia uliovunjika tangu mwaka 2016. Makubaliano kati ya nchi hizo mbili yalisimamiwa na China.
Vyanzo:DPA/AP/AFP
Mhariri: Bruce Amani