Mataifa sita yenye nguvu yaijadili Iran.
15 Aprili 2010Matangazo
Mabalozi kutoka katika nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani walikutana
katika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York katika
mkutano wao wa pili katika kipindi cha wiki, tangu China, ambayo
inauhusiano wa karibu wa kiuchumi na Iran, kukubali kujiunga katika
mazungumzo hayo.
Wanadiplomasia hao walikuwa wakijadiliana juu ya azimio la awali,
ambalo lilisambazwa wiki zilizopita, linaloandaa kuweka awamu ya
nne ya vikwazo dhidi ya Iran kutokana na kukataa kwake kuachana
na mpango wake wa kurutubisha nyuklia.
Akizungumzia na waandishi wa habari mara tu baada ya mkutano
wao huo uliochukua saa 3, balozi wa Ufaransa Gerard Araud
amesema wamefikia katika hoja ya msingi, hali inayowafanya
kusonga mbele na kufahamisha pia kwamba watafanya mikutano
mingine.
Hata hivyo hakufahamisha mkutano ujao utafanyikiwa wapi.
Naye balozi wa China Li Baodong ameelezea kuafikiana zaidi katika
mkutano huo.
Nchi za magharibi zimekuwa zikiiilaumu Iran kwamba inataka
kutengeneza silaha za nyuklia, lakini Iran yenyewe inasema kuwa
lengo la nyuklia hiyo ni kuzalisha umeme kwa ajili ya matumizi ya
raia.
Muswada huo ulioandaliwa na Marekani unapendekeza hatua mpya
za kuzibana benki za Iran, nchi hiyo kuwekewa vikwazo kamili vya
silaha, hatua kali dhidi ya biashara ya nchi hiyo ya kusafirisha kwa
meli, kupigwa marufuku kwa vitega uchumi vipya katika sekta ya
nishati ya Iran na pia hatua dhidi ya askari wa kikosi cha mapinduzi
cha nchi hiyo.
Katika mkutano wa kwanza uliofanyika Alhamisi iliyopita, ambao pia
ulihudhuriwa na mabalozi kutoka nchi hizo sita, Marekani, Uingereza,
Ujerumani, Ufaransa na Urusi, balozi wa China Li Baodong
alioneshwa kukwera na maependekezo hayo ambayo yanaathiri
sekta ya nishati ya Iran.
Rais Barack Obama wa Marekani amezishinikiza nchi zilizohudhuria
mkutano juu ya usalama wa nyuklia mjini Washington siku ya
Jumanne kuiwekea vikwazo Iran lakini alikiri kuwa China ina
wasiwasi juuu ya madhara ya kiuchumi na kusema kwamba
majadiliano ni magumu.
Mataifa ya magharibi yamekuwa yakisema kuwa uchu wa Iran kupata
silaha za nyuklia utaweza kuyumbisha kwa kiasi kikubwa eneo hilo la
mashariki ya kati.
Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters)
Mhariri: Mohammed, Abdul-Rahman
Matangazo