1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Mashambulizi makali ya Israel yailenga Rafah

Iddi Ssessanga
27 Machi 2024

Israel imefanya mashambulizi makali kusini mwa Gaza usiku wa kuamkia Jumatano, licha ya shinikizo la kimataifa la kutaka mapigano yasitishwe mara moja katika eneo hilo la Wapalestina linalokabiliwa na kitisho cha njaa.

https://p.dw.com/p/4eAcx
Mzozo wa Mashariki ya Kati | Khan Yunis
Mashambulizi ya Israel yamegeuza sehemu kubwa ya Gaza kuwa magofuPicha: Yasser Qudih/Xinhua/IMAGO

Ukanda wa Gaza uliozingirwa unakabiliwa na hali mbaya ya kiutu na Marekani imesema itaendelea na utaratibu wake wa kudondosha msaada kutokea angani, licha ya miito kutoka kwa Hamas kusitisha utaratibu huo baada ya kundi hilo kusema watu 18 walikufa wakati wanajaribu kufikia vifurushi vya chakula.

Jumanne usiku Israel ilifanya mashambulizi makali katika mji wa kusini wa Rafah, ambao ndiyo bado haujashambuliwa na vikosi vya ardhini vya Israel. Takribani watu milioni 1.5 wamerundikana katika eneo hilo, wengi wao wakiwa wamekimbilia kusini kuelekea mpaka na Misri.

Milipuko pia ilisikika na moshi kuonekana ukitanda katika mji wa Gaza City upande wa kaskazini, ambako wanajeshi wa Israel wamekuwa wakishambulia hospitali kubwa zaidi ya mji huo kwa zaidi ya wiki sasa.

Wakaazi wa Gaza waliokimbia eneo la Hospitali ya Al-Shifaa
Malefu ya wakaazi wa Gaza wanakabiliwa na kitisho cha njaaPicha: Dawoud Abo Alkas/Anadolu Agency/picture alliance

Wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas, imesema mapema Jumatano kuwa watu 66 wameuawa usiku, wakiwemo watato watatu, katika mashambulizi ya ndege za Israel ndani karibu ya Rafah.

Soma pia: Israel, Hamas zakomalia misimamo yao vita vya Gaza

Mapigano yameendelea bila kusita siku mbili baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio lake la kwanza la kutaka usitishaji mara moja wa mapigano, na kuhimiza kuwaachiliwa kwa mateka wapatao 130 ambao Israel inasema wanaendelea kushikiliwa na mjini Gaza, wakiwemo mateka 34 wanaodhaniwa kufa.

Vikosi vya Israel pia vimezingira hospitali mbili katika mji wa Khan Yunis, ambako wizara ya afaya inasema watu 12, wakiwemo baadhi ya watoto, waliuawa katika shambulizi la Israel dhidi ya kambi ya watu waliopoteza makaazi yao.

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limeonya kuwa maelfu ya watu walikuwa wamekwama katika hospitali ya Nasser mjini Khan Yunis, na kwamba maisha yao yalikuwa hatarini.

Hospitali katika Ukanda wa Gaza zaelemewa

China yatoa wito wa kutekelezwa kwa azimio la Baraza la Usalama

Siku ya Jumanne Mjumbe wa China katika Umoja wa Mataifa alisisitiza kwamba Azimio la Baraza la Usalama laazima litekelezwe, na kutoa pia wito wa kutekelezwa kwa suluhisho la mataifa mawili haraka iwezekanavyo.

Geng Shuang, naibu mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, alitoa wito huo wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu wa umoja huo mjini New York, kuhusu mzozo wa Israel na Wapalestina.

Soma pia: Baraza la Usalama lapitisha azimio la usitishaji mapigano Gaza

"Ninataka kusisitiza kwamba kila azimio la Baraza la Usalama, likiwemo azimio nambari 2728, linayo nguvu ya kisheria. Halina mashaka na haliwezi kupingwa," alisema balozi Shuang.

"Nchi inapojiunga na Umoja wa Mataifa, inaahidi kutekeleza maamuzi ya Baraza la Usalama, ambayo ni wajibu chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Marekani, kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, inapaswa kuongoza katika kutii azimio hilo," aliongeza.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameendelea kulikosoa vikali azimio la Umoja wa Mataifa, akiadai kwamba linaipa kiburi Hamas na kudhoofisha juhudi za kuwakomboa mateka, na kuapa kuendelea na operesheni zake hata kwa kubaki yenyewe tu.

Marekani | Baraza la Uslaama la UN New York | Azimio la usitishaji vita Gaza
Baraza la Usalama la UN lilipiga kura kwa mara ya kwanza na kupitisha azimio la kutaka kusitishwa mara moja kwa vita Gaza.Picha: Fatih Aktas/Anadolu/picture alliance

Hezbollah yaivurumishia Israel maroketi

Kwingineko katika mzozo huo, kundi la Hezbollah la nchini Lebanon, limesema limefanya mashambulizi ya roketi dhidi ya mji wa Kiryet Shmona nchini Israel mapema Jumatano, kujibu mashambulizi mabaya yaliofanywa na Israel kwenye kijiji cha Hebbariye kusini mwa Lebanon siku moja kabla, na kuuwa wapiganaji watatu wa Hezbollah.

Watu wasiopungua saba waliuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Hebbariyeh, vyanzo viwili vya idara za usalama za Lebanon vililiambia shirika la habari la Uingereza, Reuters.

Soma pia: Mjumbe wa Marekani aonya dhidi ya vita mpakani mwa Lebanon

Mashambulizi ya Israel yalionekana kulenga kituo cha dharura na misaada cha kundi hilo katika kijiji hicho, vilisema vyanzo hivyo.

Maafisa wa afya nchini Israel wamesema raia mmoja ameuawa katika mashambulizi ya Hezbollah.

Chanzo: Mashirika