1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yahimiza uchunguzi huru kuhusu ukiukaji AfDB

26 Mei 2020

Wizara ya fedha ya Marekani imeitaka Benki ya Maendeleo Afrika AfDB, kufanya uchunguzi huru juu ya madai ya ukiukaji wa maadili dhidi ya rais wake Akinwumi Adesina, ambaye alisafishwa awali na magavana wa benki hiyo.

https://p.dw.com/p/3cn6c
Akinwumi Adesina, neuer Präsident der Afrikanischen Entwicklungsbank
Picha: AFP/Getty Images/S. Kambou

Katika barua ambayo shirika la habari la Ufaransa, AFP limepata nakala yake siku ya Jumatatu, waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu matokeo ya uchunguzi wa ndani uliomsafisha Adesina, na kuhimiza uteuzi wa mchunguzi huru wa nje.

Barua hiyo ya tarehe 22 Mei, ilitumwa kwa mwenyekiti wa bodi ya AfDB, ambaye ni waziri wa mipango na Maendeleo wa Cote d'ivoire Niale Kaba. Adesina anawania muhula wa pili wa miaka mitano kuiongoza AfDB, mmoja ya benki tano kubwa zaidi ya maendeleo duniani.

US Finanzminister Steven Mnuchin
Waziri wa fedha wa Marekani Steve Mnuchin.Picha: AFP/N. Kamm

Mwezi uliyopita, wafichuzi waliwasilisha ripoti ya kurasa 15 kwa magavana wa benki hiyo ikiainisha madai ya ubadhirifu wa mali, upendeleo kwa raia wenzake wa Nigeria katika uteuzi wa nafasi za juu na upandishaji vyeo wa watu wanaotuhumiwa au waliotiwa hatiani kwa udanganyifu na rushwa.

Kamati ya maadili ya benki hiyo ilimsafisha kikamilifu Adesina, ikisema madai yaliotolewa dhidi yake hayakuwa na ukweli wowote. Adesina mwenyewe alipuuza madai hayo akiyataja kuwa ya uongo, yasiyo na msingi na ya uzushi.

Adesina, waziri wa zamani wa kilimo wa Nigeria mwenye umri wa miaka 60, ndiye mgombea pekee katika uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi huu wa Mei, lakini ambao sasa umeahirishwa hadi Agosti kwa sababu ya janga la virusi vya corona.

Ameungwa mkono na Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS. Mwezi Oktoba 2019, AfDB ilikusanya kiasi cha dola za Marekani bilioni 115 katika tajiriba mpya, katika operesheni iliyochukuliwa kama mafanikio binafsi ya Adesina.

Madai ya uongozi wa kidikteta

Benki hiyo imetikiswa na kuondoka kwa watendaji kadhaa wa ngazi ya juu tangu kuwasili kwake, wakilalamika juu ya kile wanachokiita mfumo wa uongozi wa kidikteta wa Adesina.

Zentrale der Afrikanischen Entwicklungsbank
Makao makuu ya Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB, yalioko Abidjan, Cote d'ivoire.Picha: AFP/Getty Images/S. Kambou

Katika barua yake kwa bodi ya magava, waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnunchin aliwahimiza kuanzisha uchunguzi wa kina kwa kutumia mchunguzi wa nje mwenye ueledi wa hali ya juu. Aliongeza kuwa kupuuza kiujumla madai bila uchunguzi stahiki utachafua sifa ya taasisi hiyo kama isiyosimamia viwango vya juu vya maadili na utawala bora.

AfDB haikuzungumzia mara moja hadharani juu ya barua hiyo. Benki hiyo ina mataifa 80 yenye hisa, ambapo 54 kati yake ni ya Afrika. Mengine yanatokea eneo la Amerika, Asia na Ulaya. Mchumi wa Cote d'ivoire aliezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema barua hiyo ilikuwa ishara ya wazi ya nia ya Marekani kumuondoa Adesina.

Chanzo: afpe