1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano na Taliban yashika kasi Afghanistan

Sylvia Mwehozi
7 Julai 2021

Waziri wa ulinzi wa Afghanistan, Bismillah Mohammadi amesema vikosi vya serikali viko katika hali nzito ya kijeshi, na kuongeza kuwa mapambano na wapiganaji wa kundi la Taliban yameshika kasi

https://p.dw.com/p/3wAJn
Afghanistan Soldaten
Picha: Nazim Qasmy/AP/picture alliance

Waziri Mohammadi amesema hayo hii leo baada ya wapiganaji wa kundi la Taliban kuushambalia mji wa Qala-i-Naw, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Badghis-kaskazini magharibi mwa nchi. Mohammadi ametoa uhakikisho kwamba vikosi vya taifa kwa kushirikiana na vikosi vya ndani vinavyoiunga mkono serikali, "vitatumia rasilimali na uwezo wake wote kuilinda nchi na watu wake".

Mapambano hayo yanakuja saa chache baada ya Marekani kutangaza kwamba mchakato wa kuviondoa vikosi vyake nchini Afghanistan umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na wakati pia serikali ya Kabul ikifanya mazungumzo na wawakilishi wa Taliban katika taifa jirani la Iran.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amekaribisha hatua ya Marekani kuondoka katika ardhi ya jirani yake upande wa mashariki lakini akaonya kwamba sasa Afghanistan inapaswa kuchukua maamuzi magumu kwa ajili ya mustakabali wa nchi.

Afghanistan Taliban
Wapiganaji wa Taliban Picha: Rahmat Gul/AP/picture alliance

Wakati huo huo, askari wapatao 300 wa Afghanistan ambao walivuka mpaka na kuingia Tajikistan wakati wakikimbia wapiganaji wa Taliban, wamerejeshwa nchini humo mapema leo. Mamia ya maafisa wa usalama walikimbilia katika mpaka wa Afghanistan na Tajikistan mwezi huu, wakiwakimbia wapiganaji wa Taliban waliokuwa wakizidi kusonga mbele eneo la Kaskazini. Hatua hiyo ilidhihirisha kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama wakati vikosi vya kigeni vikikaribia kukamilisha mchakato wa kuondoka baada ya miaka 20 ya vita na mazungumzo ya amani kukwama.

Chanzo kimoja cha usalama cha Tajikistan kimesema serikali ya Kabul ilituma ndege kadhaa katika uwanja wa ndege wa Kulob na ziliondoka usiku wa kuamkia leo zikiwa na askari 280. Wanajeshi wengine 300 wanatarajiwa kuondoka katika siku zijazo. Tajikistan imeelezea wasiwasi wa usalama katika eneo la mpaka na iko mbioni kusambaza askari karibu 20,000 kwa ajili ya kuimarisha usalama. Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amenukuliwa akisema wako tayari kumsaidia mshirika wake katika mgogoro huo wa Afghanistan.

"Tutafanya kila kitu, ikiwemo kutumia uwezo wa kambi ya kijeshi ya Urusi katika eneo la mpaka wa Tajikistan na Afghanistan ili kuzuia hatua yoyote ya kichokozi dhidi ya washirika wetu".

Kwa miezi sasa kundi la Taliban limekuwa likiizunguka miji mikuu ya mikoa kote nchini Afghanistan, huku wafuatiliaji wakitabiri kwamba wapiganaji hao wanasubiri kuondoka kikamilifu kwa vikosi vya kigeni kabla ya kufanya mashambulizi kwenye maeneo ya mijini.

Vyanzo: Reuters/AFP