1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Merkel aendelea kuwa Kansela

Daniel Gakuba
7 Desemba 2018

Annegret Kramp-Karrenbauer amepata ushindi wa kura chache kuwa mwenyekiti mpya wa chama cha CDU. Jukumu lake sasa litakuwa kuleta mageuzi yanayohitajika katika chama hicho. Ni maoni ya mhariri mkuu wa DW, Ines Pohl.

https://p.dw.com/p/39gzk
Deutschland CDU-Parteitag in Hamburg Kramp-Karrenbauer
Annegret Kramp-Karrenbauer, mwenyekiti mpya wa chama cha CDUPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Sio kawaida kwa vyombo vya habari vya kimataifa kujishughulisha na mtu anayechaguliwa kukiongoza chama cha kisiasa nchini Ujerumani, lakini mara hii, hali imekuwa tofauti. Magazeti maarufu kama vile the New York Times la Marekani yameupa umuhimu mkubwa mkutano mkuu wa chama cha CDU, kuliko mazishi ya rais wa zamani wa nchi hiyo George H.W. Bush. Vyombo vikubwa vya kimataifa vimetangaza mara moja matokeo ya uchaguzi wa mwenyekiti wa chama hivyo. Sababu ya yote haya, na Angela Merkel.

Kwa watu wengi, Kansela huyo wa Ujerumani ndiye kiongozi muhimu zaidi duniani. Wakati viongozi wengine kama Donald Trump wa Marekani, Vladimir Putin wa Urusi na Recep Tayyip Erdogan wakishindana kwa ubabe, Merkel amekuwa mtulivu, mwenye sauti ya mwisho ya kuweka uzani katika dunia inayokabiliwa na hatari ya migawanyiko ya itakanayo na sera za utaifa.

Hata hivyo, nchini mwake haiba ya Merkel imedhoofika. Hayo yamedhihirika katika matokeo mabaya ya uchaguzi katika jimbo moja baada ya jingine, na sauti za ukosoaji ambazo zinazidi kupazwa ndani ya chama chake mwenyewe. Kwa hali hiyo Bi Merkel hakuwa na chagua jingine bali kuachia uongozi wa chama, na tangazo lake mwezi Oktoba la kujiweka kando, lilifuatiwa na kinyang'anyiro kikali  cha kutaka kumrithi.

Kisasi cha mtu aliyejeruhiwa.

Ingawa bado muhula wake wa ukansela unabakisha miaka miwili na nusu, ilikuwa bayana kwamba ingekuwa vigumu kuukamilisha, kama angechaguliwa hasimu wake kisiasa.

Ines Pohl Kommentarbild App
Ines Pohl, Mhariri mkuu wa DWPicha: DW/P. Böll

Na karibu hilo litokee. Friedrich Merz, mwanamme ambaye Merkel alimfurusha katika siasa miaka minane iliyopita, alishindwa katika duru ya pili, tena kwa tofauti ya kura 35, kati ya 999 zilizopigwa. Tangu asubuhi, hali ya hewa ilikuwa na muungurumo wa ulipizaji kisiasi, kutoka kwa wanaume wengi ambao Angela Merkel amewajeruhi kisiasa, wakimuunga mkono Merz.

Matokeo yalipotangazwa baada ya siku ndefu iliyoanza na hotuba iliyojaa hisia ya Kansela Merkel, mshindi alikuwa Annegret Kramp-Karrenbauer. Kwa matokeo hayo, chama cha CDU kimemwidhinisha Merkel kuumaliza muhula wake wa ukansela, ikiwa chama cha SPD kinachoshiriki katika serikali ya mseto hakitajiondoa.

Ujerumani kuendelea kuwa tegemeo katika sera za kimataifa

Kwenye uwanja wa kimataifa, inamaanisha kwamba Ujerumani itaendelea kuwa ya kutegemewa, na msimamo wake katika Umoja wa Ulaya hautabadilika sana. Nyumbani, Kramp-Karrenbauer atafuatiliwa kwa ukaribu, namna atakavyoweza kuganga roho ya chama chake, na kuzileta pamoja kambi mbali mbali. Atatazamwa pia jinsi anavyoleta mwamko mpya, si tu katika chama chake cha CDU, bali pia kwa Ujerumani, na kuweza kushinda uchaguzi mkuu ujao, unaoweza kuja baaya ya Kansela Merkel kakaa madarakani kwa miaka 16.

Kimsingi itakuwa kuangalia kama Kramp-Karrenbauer ataweza kujinasua katika ushawishi wa mkubwa wake, na kuwa huru katika kupata uzoefu wa kimataifa, ambao utamweka katika nafasi nzuri ya kugombea ukansela. Hayo ni masuala ya baadaye, lakini kwa sasa, chama cha CDU hakina mwanamke mmoja kileleni, kinao wawili.

Mwandishi: Ines Pohl

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri: Thomas Latschan