1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maharamia waiteka meli katika pwani ya Somalia

Josephat Charo
14 Machi 2017

Maharamia wa kisomali wameiteka meli iliyosheheni mafuta iliyokuwa njiani kuelekea katika bandari ya Alula nchini Somalia ikitokea Sri Lanka.

https://p.dw.com/p/2Z8AN
Somalischer Pirat Somalia
Picha: picture alliance/AP Photo/F.Abdi Warsameh

Mtaalamu mmoja wa masuala ya uhamiaji amesema meli hiyo ilituma ujumbe kuonya ilikabiliwa na matatizo, ikazima mfumo wake wa ufuatiliaji na kubadili mkondo wa safari kuelekea pwani ya Somalia.

Maafisa wa Somalia na wataalamu wa masuala ya uharamia wamethibitisha kutekwa kwa meli hiyo, hiki kikiwa kisa cha kwanza cha utekaji wa meli kubwa ya kibiashara kufanywa na maharamia wa kisomali tangu 2012. Mtaalamu wa masuala ya uharamia wa shirika la Oceans Beyond Piracy, John Steed, amesema meli hiyo kwa jina Aris 13 ilikuwa imebeba mafuta kutoka Djibouti kuelekea mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na ilikuwa na wafanyakazi wanane raia wa Sri Lanka.

Steed, ambaye ni kanali wa zamani wa jeshi la Uingereza, amejishughulisha na masuala ya uharamia kwa karibu muongo mmoja na ana mawasiliano ya karibu na vikosi vya baharini vinavyoifuatilia meli hiyo. Ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa meli hiyo iliripoti siku ya Jumatatu(13.03.2017) mchana ilikuwa ikifuatiliwa na boti mbili ndogo, kisha ikatoweka. Steed aidha amesema meli hiyo ilikuwa njiani ikielekea bandari ya Alula nchini Somalia.

Meli yatia nanga bandarini

Salad Nur, mmoja wa viongozi wazee wa eneo hilo ameliambia shirika la habari la Associated Press kwa njia ya simu kwamba meli hiyo tayari imetia nanga katika bandari hiyo. Nur aidha amesema wanaume zaidi waliokuwa na silaha wameingia ndani ya meli hiyo. Afisa mmoja anayefanya shughuli zake Mashariki ya Kati anayefahamu kuhusu tukio hilo pia ameliambia shirika hilo la habari kuwa mpaka sasa hakuna fidia yoyote iliyodaiwa na maharamia hao.

Indischer Ozean Piraten überfallen chinesisches Schiff
Maharamia wa Kisomali walipoiteka meli ya China (17.11.2008)Picha: picture-alliance/dpa/J. Zalasky

Afisa wa jimbo la Puntland amesema awali wanaume kadhaa waliingia ndani ya meli hiyo kaskazini mwa pwani ya Somalia, eneo linalofahamika sana kutumiwa na wasafirishaji wa silaha na wanachama wa kundi la wanamgambo la al Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.

Kwa mujibu wa data za mtandao wa Equasisi unaokusanya taarifa za safari za meli unaosimamiwa na wizara ya usafiri ya Ufaransa, meli hiyo yenye uzito wa tani 1,800 inamilikiwa na kampuni ya meli ya Armi ya Panama na inasimamiwa na kampuni ya usimamizi wa meli ya Aurora ya Dubai, katika Falme za Kiarabu.

Noel Choong, Mkuu wa kituo cha kimataifa cha kuripoti matukio ya uharamia mjini Kuala Lumpur amesema meli ya Aris 13 ilikuwa ikifuatiliwa na shirika la biashara la safari za baharini la Uingereza, linaloratibu usimamizi wa meli na boti za kibiashara katika eneo la ghuba ya Aden. Hata hivyo ofisi ya shirika hilo huko Dubai imesema haikuwa na taarifa zaidi kuhusu utekaji wa meli hiyo kwa sasa.

Kikosi cha Umoja wa Ulaya chafanya uchunguzi

Wakati haya yakiarifiwa kikosi maalumu cha kupambana na uharamia cha Umoja wa Ulaya, EU Navfor, kimetuma ndege katika pwani ya Somalia kuchunguza taarifa kuhusu maharamia wa kisomali kuiteka meli ya Aris 13. Akizungumza na shrika la hbari la Ujerumani dpa msemaji wa kikosi hicho amesema, "Ndege iko njiani. Hatufahamu kilichotokea. Hatukiorodheshi kama kisa cha uharamia kwa wakati huu."

Kriegsschiff der EU NAVFOR Mission
Meli za kikosi cha EU Navfor kinachopambana na uharamia pwani ya SomaliaPicha: www.eunavfor.eu

Msemaji wa kikosi cha EU Navfor pia amesema meli hiyo ilianza safari yake nchini Sri Lanka, lakini hakuweza kuthibitisha ripoti kwamba ilikuwa ikibeba mafuta kuyapeleka nchini Somalia. Kikosi hicho hufanya operesheni dhidi ya uharamia katika pwani ya Somalia ambako uharamia ulishamiri mpaka pale usalama ulipoimarishwa 2012.

Wakati wa kilele cha uharamia miaka mitano iliyopita, maharamia wa kisomali waliwahangaisha mabaharia waliovuka ghuba ya Aden. Shirika la Kimataifa la safari za baharini linasema maharamia hao waalifanya mashambulizi 237 katika pwani ya Somalia mwaka 2011 na kuwazuilia mamia ya mateka. Lakini mashambulizi yalipungua kwa asilimia kubwa baada ya wamiliki wa meli kuimarisha usalama na kuiepuka pwani ya Somalia.

Mwandishi:Josephat Charo/reuters/dpaa/ape

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman