1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron: Calais kutokuwa na kambi nyingine ya wahamiaji

Grace Kabogo
16 Januari 2018

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ameapa kuwa nchi yake haitoruhusu kuanzishwa kambi nyingine ya wahamiaji Calais na ameishinikiza Uingereza kutoa majibu kwa Ufaransa kuhusu watoto ambao hawana watu wa kuwasindikiza.

https://p.dw.com/p/2qwEB
Frankreich Emmanuel Macron in Calais
Picha: picture-alliance/dpa/MAXPPP/J.B. Azzouz

Akizungumza leo katika mji wa kaskazini wa Calais, Macron amesema hatoruhusu kuanzishwa kwa kambi nyingine ya wahamiaji ya msituni kama iliyokuwepo hapo kabla. Amesema serikali yake inazidi kuweka shinikizo kwa Uingereza kuchangia zaidi katika kukabiliana na wahamiaji wanaotaka kuvuka mpaka.

Amesema wanajitahidi kufanya kila linalowezekana kuwazuia watu kuvuka mpaka kinyume cha sheria na kwamba Calais isitumike kama mlango wa kuingia Uingereza. Serikali ya mtangulizi wa Macron, Francois Hollande iliivunja kambi ya msituni ya Calais ambayo ilikuwa ikiwahifadhi kiasi ya watu 100,000 hadi Oktoba mwaka 2016.

Macron amesema wanapaswa kusimamia vizuri suala la watoto wasio na watu wa kuwasindikiza, kuimarisha ushirikiano wa polisi katika eneo la Calais na nchi wanazotoka wahamiaji hao pamoja na kuruhusu fedha kwa ajili ya kusaidia miradi muhimu ya maendeleo ya watu wa Calais. Amesema hayo ni masuala makuu matatu atakayozungumza na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May siku ya Alhamisi.

Nitafikisha ujumbe kwa Theresa May

''Niko mbele yenu, siku mbili kabla ya mkutano wa kilele kati ya Ufaransa na Uingereza. Ni muhimu kuja kujionea uzoefu wa kile kinachoendelea hapa kwa miezi kadhaa, miaka kadhaa na kufikisha ujumbe kwa Theresa May katika muda wa saa 48 zijazo kuhusu masuala kadhaa ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi katika usimamizi wetu wa kawaida,'' alisema Macron.

Migranten in Calais beim gemeinsamen Mittagessen
Wahamiaji katika kambi ya CalaisPicha: DW/D.Pundy

Hata hivyo, mamia ya watu wanaendelea kuweka kambi Calais, wakiwa na matumaini ya kudandia malori yanayoenda Uingireza, nchi ambayo baadhi ya wahamiaji kutoka Afghanistan na Afrika Mashariki wanaiona kama sehemu nzuri ya kuishi. Macron amewataka polisi kutotumia nguvu kubwa dhidi ya wahamiaji, lakini amevitetea vikosi vya usalama dhidi ya madai ya ukatili wanaoufanya, ambayo yametolewa na baadhi ya mashirika ya kutoa misaada, akiyapuuza mengine kuwa ya uwongo. Hata hivyo, amewasihi polisi kuwachukulia vizuri watu ambao wamekimbia vita na umasikini na kwenda kutafuta maisha bora.

Ufaransa inaitaka Uingereza kuchangia katika mzigo mkubwa wa gharama za usalama katika eneo la mpakani na kuwachukua zaidi watu wanaoomba hifadhi. Aidha, ameshutumu taarifa za matumizi ya mabomu ya kutoa machozi na ukatili wa kimwili dhidi ya wahamiaji, pamoja na madai kwamba wahamiaji wanapokonywa mali zao, akisema jambo hilo halitoruhusiwa.

Macron aliwaagiza maafisa wa Ufaransa kumpa maelezo kuhusu uharakishwaji wa mchakato kwa wahamiaji ambao wanakubali kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini Ufaransa. Mkurugenzi wa shirika linalovisimamia vituo vitatu vya wahamiaji katika mkoa wa Calais, Guillaume Alexandre, amesema karibu asilimia 70 ya wahamiaji wanaondoka bila ya kujaza makaratasi yoyote nchini Ufaransa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga