Macedonia yatumbukia kwenye mgogoro mzito | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.04.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Vurugu Macedonia

Macedonia yatumbukia kwenye mgogoro mzito

Macedonia imetumbukia katika mpasuko na mgawanyiko mkubwa wa kikabila kundi la Waalbania waliochache likilengwa

Kiongozi wa upinzani nchini Macedonia ameukataa mwito uliotolewa na rais wa nchi hiyo wa kufanyika mazungumzo ya dharura kati ya viongozi wa chama ikiwa ni masaa kadhaa baada ya waandamanaji wengi wao wakiwa ni wafuasi wa chama tawala cha kihafidhina kulivamia bunge na kuwashambulia wabunge wa upinzani.

Taarifa zilizotolewa na afisa mmoja wa chama cha Social Demokratic zinasema kwamba kiongozi mkuu wa upinzani, Zoran Zaev, hatohudhuria mazungumzo, lakini hakutowa maelezo zaidi kuhusiana na hilo. Afisa huyo hakutaka kutajwa jina kwa sababu hana mamlaka ya kulizungumzia suala hilo mbele ya waandishi habari.

Polisi inasema watu 102 wamejeruhiwa wengi wakiondoka na majeraha madogo kufuatia vurugu zilizozuka.Zaev ni miongoni mwa wahanga wa vurugu hizo pamoja na kiongozi wa chama kingine kidogo cha upinzani cha  waalbania na maafisa 22 wa polisi pia wameumizwa. Rais wa nchi hiyo, Gjorge Ivanov, ametowa mwito wa utulivu kwa kusema:

"Kila mmoja anapaswa kubeba dhamana ya vitendo vyake na kila mtu anapswa kutambua juu ya hatua zitakazochukuliwa kutokana na hili. Hii ni hali inayoweza kupatiwa ufumbuzi kwa misingi ya kuheshimu mfumo wa sheria wa Jamhuri ya Macedonia."

Macedonia iko katika dimbwi la mgogoro mkubwa wa kisiasa ulioanza na kadhia ya udukuzi  wa mawasiliano ya simu miaka miwili iliyopita  pamoja na uchaguzi ambao haukukamilika mwaka jana ukazidi kuitumbukiza hali katika mvurugano. Waziri wa mambo ya ndani amejiuzulu.

Mazedonian Präsident Gjorge Ivanov PK (picture-alliance/abaca/A. Fazlagikj )

Rais Gjorge Ivanov

Taifa hilo la kusini mashariki mwa Ulaya, Macedonia pia linazidi kugawika kwa misingi ya kikabila huku waandamanaji wakipinga mipango ya upinzani ya kutaka kutoa madaraka makubwa zaidi  kwa Waalbania walio wachache, ambao ni robo ya idadi jumla ya wananchi wa taifa hilo.

Umoja wa Ulaya umelaani vurugu na ghasia za alhamisi mkuu wa seza za nje wa Umoja huo Federico Mogherini amesema  msingi wa demokrasia unapaswa kuheshimiwa.

''Tunazichukulia vurugu siku zote kuwa ni kitu kisichokubalika na hasa zinapotokea katika nyumba ya demokrasia,bungeni na sisi tunaamini kwamba  kila mmoja mjini Skopje anabidi kuiheshimu katiba na demokrasia na kujaribu kuiondoa nchi katika mgogoro huu mkubwa unaoweza kuwa hatari.''

Katika nchi jirani ya Serbia, Waziri Mkuu Aleksander Vucic ameitisha mkutano wa dharura  juu ya usalama kutokana na vurugu hizo.

Kadhalika kiongozi wa chama cha kihafidhina, Nikola Gruevski, amelaani ghaisa hizo lakini anasema mahasimu wake kisiasa ndio waanzilisshi wa chokochoko. Akizungumza katika makao makuu ya chama chake leo hii Gruevski alisema chama cha Social Democrats wamevunja sheria na katiba kwa kumchagua spika mpya wa bunge ambae ni mwanasiasa kutoka kabila la Waalbania licha ya kuwepo mvutano kwa miezi kadhaa katika juhudi za kuunda serikali mpya nchini humo.

Urusi inasema kwamba Umoja wa Ulaya na Marekani ndio fitna wakubwa katika mgogoro huo. Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imetowa taarifa leo ikisema nchi za Magharibi ndio waingiliaji wakubwa wa mambo ya ndani ya Macedonia na ndio chanzo kikubwa cha mgogoro wa kisiasa  nchini humo.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com