Maandamano ya kumpinga Trump yazuka Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Maandamano ya kumpinga Trump yazuka Marekani

Rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kukutana na Trump katika Ikulu ya White House kujadili mchakato wa kupokezana madaraka

Rais Barack Obama anatarajiwa kumkaribisha rasmi rais mteule Donald Trump katika ikulu ya Whitehouse leo, mnamo wakati maelfu ya raia wa Marekani wameandamana katika majimbo mengi nchini humo kupinga ushindi wa bilionea huyo. Katika maeneo mengine waandamanaji wameziba barabara hivyo kutatiza shughuli za usafiri na kulazimisha polisi kutumia gesi za kutoa machozi. Miongoni mwa miji ambayo maandamano yamefanyika ni New York, Los Angeles, Carlifornia na Oakland. 

Wakiwa wamebeba mabango ambayo yameandikwa kwa kiingereza "Not my President"  yaani si rais wangu, na wengine kuteketeza moto sanamu ya kichwa cha Donald Trump, maelfu ya waandamanaji hao wamepinga ushindi wa Trump wakishutumu kauli zake wakati wa kampeni ambazo wanasema zinabagua wahamiaji, Waislamu na makundi mengine. Muandamanaji mmoja ambaye hakujitambulisha jina alisema "Ni mbaguzi wa rangi, ni dhalimu wa kimapenzi, mnazi mamboleo. Hapaswi kuongoza nchi yetu".

Katika jimbo la New York, maelfu ya wanadamanaji walijaza barabara katikati ya jiji la Manhattan wakielekea katika jingo la gorofa la Trump Tower.

Waandamanaji Chikago wapinga ushindi wa Trump

Waandamanaji Chikago wapinga ushindi wa Trump

Katika jimbo la Los Angeles, zaidi ya waandamanaji elfu tano walijitokeza miongoni mwao wanafunzi. Wakaketi katika barabara kuu mbili za kuingia mji huo hivyo kutatiza usafiri. Waandamanaji kumi na watatu walikamatwa polisi ilipokuwa ikiwatawanya. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari nchini humo CBS.

Hali sawa na hiyo imejitokeza Oakland Carlifornia ambapo zaidi ya waandamanaji 6000 waliziba barabara. Maafisa wa polisi waliwakabili kwa kutumia kemikali za kuwasha ngozi. Maafisa wawili wa polisi walijeruhiwa huku magari mawili ya polisi yakiharibiwa.

Maandamano hayo yameshuhudiwa Chikago, Seatle, Philadelphia, Boston na maeneo mengine mengi Marekani. Muandamanaji mwengine ambaye pia hakujitambulisha jina amesema "Ninaandamana kuwakomboa wamarekani dhidi ya ukandamizaji kutoka kwa mtu wa kutisha."

Hayo yakijiri, rais Barrack obama anatarajiwa kumkaribisha rais mteule Donald Trump katika ikulu ya White House leo. Mkutano huo unaashiria mwanzo wa mchakato wa mpito wa kupokezana mamlaka. Trump anatarajiwa kuapishwa Januari 20 na achukue rasmi urais kutoka kwa Obama. Obama aliongoza kampeni ya kumpinga Trump wakati wa kampeni lakini kwenye hotuba yake baada ya matokeo ya kura, alimpongeza Trump na kuwahimiza wamarekani kushirikiana naye. Wakati wa kampeni, Trump aliahidi kufutilia mbali baadhi ya miradi iliyoanzishwa na Obama mfano bima ya Afya ijulikanayo kama Obama Care

Mwandishi: John Juma/RTRE/APE/DPE
Mhariri:Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com