1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano kupinga unazi mambo leo yafanyika Marekani

Isaac Gamba
13 Agosti 2018

Maelfu ya watu waliokuwa wakitaka kutuma ujumbe kuashiria kwamba ubaguzi wa rangi hauna nafasi nchini Marekani walikusanyika hapo jana nje ya ikulu ya Marekani White House.

https://p.dw.com/p/334IL
USA, Washington: Demonstrationen zum Charlottesville-Jahrestag
Picha: picture-alliance/L. Vogel

Maandamano hayo yaliyofanyika katika miji ya Charlotteville na Washington  yalikuwa ya amani licha ya mtu mmoja kukamatwa mjini Washington na wengine wanne walikamatwa mjini Charlottesville.

Mjini Charlottesville mama wa mtoto aliyeuawa wakati wa maandamano yaliyofanyika katika msimu wa majira ya kiangazi mwaka jana alizuru eneo la shambulizi akisema majeraha yaliyotokana na matukio ya ubaguzi wa rangi bado hayajapona

Mjini Washington  katika maeneo ya ikulu ya Marekani White House polisi kadhaa waliwadhibiti waandandamanaji wanaounga mkono siasa kali za mrengo wa kulia  ili wasiwazomee waandamanaji wanaopinga uzalendo mambo leo.

Jasson Kessler, muandaaji wa maandamano ya mwaka jana  ya watu wanaotetea uzalendo mambo leo aliongoza maandamano ya hapo jana  aliyoyaita haki ya mtu mweupe . Kessler katika barua yake ya kuomba kibali cha maandamano alisema alitarajia watu 100 hadi 400 wajitokeze kushiriki lakini hata hivyo  ni watu waliojitokeza walikuwa wachache sana wakikadiriwa kufikia 20.

 

Hata hivyo maandamano hayo yaliingiliwa na maelfu ya waandamanaji waliokuwa wakipinga uzalendo mambo leo waliokuwa wamekusanyika hapo kabla katika viwanja vya Lafayette .  Makia Green anayewakilisha kundi la watu weusi mjini Washington chini ya kauli mbiu " Maisha ya Mtu Mweusi ni MuhImu" alisikika akisema licha ya yote  bado wanatambua kutokana na uzoefu wao kuwa kupinga uzalendo mambo leo ni suala lisilo itikiwa vizuri nchini humo.

 

 Rais Donald Trump hakuwepo ikulu

UK Boris Johnson
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: picture-alliance/empics/V. Jones

Rais Donald Trump ambaye alichochea mivutano zaidi kutokana na kauli yake wakati akizungumzia vurugu za mwaka jana za Chalottesville alipozilaumu pande zote mbili safari hii hakuwa katika makazi yake ya Ikulu kwani alikuwa katika mapumziko ya kikazi mjini New Jersey  katika kipindi cha zaidi ya wiki moja sasa.

Mkuu wa polisi mjini Washington Peter Newsham  aliwapongeza maafisa wake kwa kufanikiwa kuzuia vurugu ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kuyatenganisha makundi hayo mawili yenye itikadi tofauti yaliyokuwa yakiandamana.  Alisikika akisema wametumia utaratibu mzuri katika kulinda usalama wa watu na mali zao ikiwa ni pamoja na kuruhusu raia kutumia haki yao ya kuandamana na kujieleza.

Mapema mjini Charlottesville mama wa binti Heather  Heyer aliyeuawa wakati wa maandamano ya mwaka jana alisema bado kuna mengi ya kufanya katika kuponya majeraha  yaliyosababishwa na vurugu za mwaka jana. Mama huyo Suzan Bro aliweka shada la maua  katika eneo ambalo vurugu zilifanyika mjini Charlottesville na kuwashukuru watu walioungana naye kumkumbuka binti yake wakati wa tukio hilo.

Alisikika akisema kuna kazi kubwa ya kufanya katika kutibu majeraha ya vurugu zinazotokana na matukio ya ubaguzi na kusema kuna haja ya kulitafutia ufumbuzia haraka tatizo hilo vinginevyo tutarejea kulekule.

Mamia ya  Wanazi mamboleo, na  wanachama  wa  kundi linaloangalia  jamii  ya  wazungu  kuwa  bora  zaidi  la  Ku Klux Klan na wengine wafuasi wa  siasa  za  kizalendo  walikusanyika  katika mji  wa  Charlottesville  Agosti 12 , 2017, kwa  sehemu  fulani kupinga  uamuzi  wa  mji  huo  kuliondoa  sanamu  la  kumbukumbu ya jenerali Robert  E. Lee kutoka  katika  uwanja  wa  mji  huo.

Makabiliano  makali  yalizuka  baina  ya  waliohudhuria dhidi ya maandamano  ya   kupinga. Maafisa  hatimaye  walifanikiwa kulilazimisha  kundi hilo  kutawanyika, lakini  ghasia  zilizuka tena wakati  gari ilipogonga  kundi  la waandamanaji.

Mwandishi: Isaac Gamba /APE

Mhariri: Josephat Charo