Korea ya Kaskazini yaweka majeshi katika hali ya mapambano | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Korea ya Kaskazini yaweka majeshi katika hali ya mapambano

Korea ya Kaskazini imewaamuru wanajeshi wake walioko mstari wa mbele kuwa tayari kimapambano, ili kuishinikiza Korea ya Kusini iache kuvitumia vipaza sauti kutangaza propaganda dhidi ya Korea ya Kaskazini.

Kim Jong- Un aongoza mkutano wa kamati ya kijeshi

Kim Jong- Un aongoza mkutano wa kamati ya kijeshi

Kim Jong- Un amesema ikiwa Korea ya Kusini haitaviondoa vipaza sauti hivyo itashambuliwa kijeshi.

Hatua ya kiongozi wa Korea ya Kaskazini imekuja wakati ambapo mvutano wa kijeshi baina ya nchi mbili za Korea umezidi mkubwa baada ya kushambiliana kwa mizinga hapo jana na kusababisha jeshi la Korea ya Kusini liwekwe katika hali ya tahadhari ya kiwango cha juu kabisa.

Kiongozi wa Korea ya Kaskazini ameshawahi kutoa amri za ushari kama hiyo mnamo miaka ya nyuma. Miaka miwili iliyopita Kim Jong -Un alitangaza hali ya kuwa vitani na Korea ya Kusini

Kim aliongoza mkutano hapo jana wa kamati kuu ya kijeshi ya nchi yake yenye mamlaka makubwa .Kamati hiyo iliiuitisha uamuzi wa kuipa Korea ya Kusini amri ya kuviondoa vipaza sauti vyake hadi ifikapo kesho alasiri (Jumamosi).

Korea ya Kaskazini haina ukweli

Schusswechsel Südkorea Nordkorea Soldaten Archiv Manöver Symbolbild

Korea ya Kusini ikifyatua makombora kujibu maroketi yaliyovurumiswha na Korea ya Kaskazini

Msemaji wa wizara ya Korea ya Kusini inayoshughulikia masuala ya kuziunganisha tena Korea mbili Jeong Joon - hee amesema Korea ya Kaskazini haina ukweli.Amesema Korea ya Kaskazini inakanusha kutega mabomu na kufanya mashambulio ya mizinga.

Msemaji huyo Jeong Joon- hee ameeleza kuwa Korea ya Kusini itapunguza idadi ya watu inaowaruhusu kwenda kwenye sehemu ya pamoja ya viwanda ya Kaesong iliyopo Korea ya Kaskazini kama ,hatua ya tahadhari. Kampuni 124 za Korea ya Kusini zinaendesha shughuli katika sehemu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Korea ya Kaskazini, kiongozi wa nchi hiyo amewaamuru wanajeshi waliopo mstari wa mbele kuwamo katika hali ya kivita kuanzia saa 11 leo. Shirika hilo la habari limemnukulu kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong -Un akiyaamuru majeshi yake yawe tayari kwa mapambano.

Lakini mkuu wa majeshi ya Korea ya Kusini amejibu kwa kuwasilisha ujumbe kwa majeshi ya Korea ya Kaskazini kuyataka majeshi hayo kutochukua hatua za hatari na kwamba Korea ya Kusini itajibu uchokozi wowote kwa nguvu zote.

Wizara ya ulinzi ya Korea ya Kusini imelipinga shinikizo la Korea ya Kaskazini juu ya kuacha kuvitumia vipaza sauti hadi ifikapo saa 11 hapo kesho. Marekani imeitaka Korea ya Kaskazini iepuke vitendo vinavyoweza kuufanya mvutano uwe mkubwa zaidi, na wizara ya ulinzi ya Marekeni imesema ipo tayari kumlinda mshirika wake Korea ya Kusini.

Mwandishi:Mtullya Abdu. afpe,dpa,

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com