1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kusini kuiongoza Interpol, imemshinda mgombea wa Urusi

21 Novemba 2018

Kuchaguliwa kwa Kim Jong Yang kumekuja kama mshangao kwa Urusi, ambayo mgombea wake Alexander Prokopchuk alikuwa ameonekana kuwa kifua mbele katika kinyang'anyiro hicho.

https://p.dw.com/p/38f44
Interpol Logo
Picha: Getty Images/AFP/R. Rahman

Wanachama wa Interpol wamemchagua Kim Jong Yang kuwa Rais mpya wa shirika hilo leo, na kupiga kura dhidi ya mgombea aliyekuwa akipigiwa upatu kushinda. Kim alikuwa kaimu rais wa shirika hilo, jukumu ambalo alichukua mwezi Septemba baada ya rais wa awali Meng Hongwei kutoweka nchini China. Idara za usalama China zinasema kwamba Meng anazuiliwa kwa makosa ya ufisadi, na kudai alijiuzulu wadhifa wake.

Kim alichaguliwa mjini Dubai wakati wa mkutano wa kila mwaka wa shirika hilo. Ataliongoza shirika hilo hadi mwisho wa muhula wa Meng unaokamilika mwaka 2020.

Südkorea Kim Jong Yang
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Kyung-kook

Kulingana na mtandao wa twitter wa Interpol, Kim alihutubia kwenye mkutano huo wa Dubai na kusema,"dunia inakabiliwa na mabadiliko yasiyotarajiwa ambayo yanasababisha changamoto kubwa kwa usalama wa umma. Ili kuyakabili matatizo hayo, lazima tuwe na mtazamo wa wazi. Tunahitaji kujenga daraja kwa maisha ya baadaye."

Ugombeaji wa Naibu Rais wa shirika hilo Alexander Prokopchuk, ambaye alikuwa mkuu katika wizara ya mambo ya ndani ya Urusi, ulisababisha ukosoaji mkubwa wa kimataifa ambao waliitaka Interpol kutompandisha cheo, kwani ukaribu wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin ulionekana kuwa tishio kwa shirika hilo.

Wanachama wa shirika hilo ambao hawana uhusiano mzuri na Urusi, wakiwemo Ukraine, Lithuania na Estonia, pamoja na maseneta wa Marekani na makundi ya upinzani ya Urusi, walikuwa wameonya kwamba kumchagua Prokopchuk's huenda kungesababisha Urusi kuitumia vibaya Interpol kuwaandama wapinzani wa kisiasa.

Alexander Prokopchuk Interpol Büro Russland
Naibu Rais wa shirika hilo Alexander ProkopchukPicha: picture-alliance/dpa/TASS/V. Sharifulin

Ikulu ya Urusi Kremlin, imekosoa shinikizo ambazo zilitolewa kupinga ugombea wa Prokopchuk. Kulingana na mashirika ya habari ya Urusi, msemaji Dmitry Peskov aliwaambia wanahabari kuwa Kremlin ilihuzunishwa na hatua ya mgombea wao kushindwa.

Ukraine ambayo ilitishia kujiondoa katika shirika hilo iwapo Prokopchuk angehaguliwa, ilipongeza uteuzi wa Kim. Waziri wa masuala ya ndani wa Ukraine ameutaja ushindi wa Kim kuwa ushindi kwa nchi yake.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/DW

Mhariri: Iddi Ssessanga