1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLebanon

Je, kundi la Hezbollah liliundwa vipi?

8 Januari 2024

Kundi la Hezbollah limekita mizizi nchini Lebanon na limejipanga kisiasa na kijeshi. Jukumu lake katika mzozo kati ya Israel na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza linaweza kuongezeka baada ya kifo cha Saleh al-Arouri.

https://p.dw.com/p/4ay0x
Hassan Nasrallah
Kiongozi wa kundi la Hezbollah Hassan NasrallahPicha: picture alliance/AP/H. Malla

Saleh al-Arouri alikuwa naibu kiongozi wa kundi la Hamas na aliuawa kwa shambulio la ndege isiyo na rubani mjini Beirut siku ya Jumanne. Al-Arouri alikuwa afisa muhimu wa Hamas na hata Hezbollah, makundi mawili yanayoungwa mkono na Iran na ambayo yameorodheshwa na Israel, Marekani, Ujerumani na mataifa mengine kadhaa ya Magharibi kuwa makundi ya kigaidi.

Ingawa hakuna aliyedai kuhusika na shambulio hilo, ambalo pia liliwaua maafisa wengine kadhaa wa Hamas, Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati, amelitaja shambulio hilo kuwa ni "uhalifu mpya wa Israeli unaolenga kuitumbukiza Lebanon katika hatua mpya ya makabiliano."

Soma pia: Israel, Hizbullah washambuliana tena 

Israel hadi sasa haijazungumzia chochote juu ya tukio hilo, lakini Mark Regev, mshauri wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amesema kuwa yeyote aliyefanya shambulio hilo hakuilenga Lebanon wala Hezbollah, bali Hamas.

Kifo cha al- Arouri kinaweza kuwa kilichovuka mpaka kwa Hezbollah ambapo kiongozi wa kundi hilo la Waislamu wa madhehebu ya Shia, Hassan Nasrallah, ameapa mara kwa mara kuwa angeishambulia Israel iwapo jeshi la nchi hiyo litawalenga maafisa wa Palestina nchini Lebanon. Jambo linaloibua wasiwasi wa mzozo huo kutanuka katika maeneo mengine ya Mashariki ya Kati.

Je, unaifahamu Hezbollah?

Wafuasi wa Hezbollah wakifuatilia hotuba kwa njia ya televisheni ya kiongozi wao Sayyed Hassan Nasrallah
Wafuasi wa Hezbollah wakifuatilia hotuba kwa njia ya televisheni ya kiongozi wao Sayyed Hassan NasrallahPicha: Mohamed Azakir/REUTERS

Hezbollah ni kundi linalofadhiliwa na Iran lenye makao yake nchini Lebanon ambako pia lilianzishwa. Jina lake linamaanisha "Chama cha Mungu". Tawi lake la kijeshi lililitajwa mwaka 2022 na kituo cha Wilson cha Marekani kuwa ni imara na kitisho kikubwa katika Mashariki ya Kati na hata ulimwenguni.

Kiongozi wa kundi hilo ni Hassan Nasrallah, ambaye amekuwa akijigamba kuwa Hezbollah ina wapiganaji karibu 100,000. Walakini, makadirio mengine ya wataalam yanaonyesha kuwa idadi hiyo inaweza kuwa chini ya hapo.

Soma pia:  Hezbollah yafyetua makombora kuelekea Israel

Mbali na harakati za kijeshi, Hezbollah inajihusisha pia katika shughuli za kisiasa na kijamii nchini Lebanon. Kutokana na kwamba theluthi moja ya Walebanon ni kutoka madhehebu ya Shia, asilimia 89 ya watu walikuwa na maoni chanya juu ya Hezbollah katika matokeo ya kura ya maoni ya mwaka 2020. Hata hivyo, Walebanon wengine wanalipinga kundi hilo, wakisema linaielekeza nchi yao katika hali ya migogoro.

Je, Hezbollah iliundwa vipi?

Kundi la Hezbollah lilianzishwa mwaka 1982 wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon vilivyodumu kwa miaka 15.

Mzozo huo ulioanza mwaka 1975, ulisababisha jamii mbalimbali za Lebanon wakiwemo Waislamu, Wakristo, watu wa mrengo wa kushoto na wazalendo wa Kiarabu kuzozana. Syria na makundi yenye silaha ya Wapalestina yalihusika pia wakati huo.

Soma pia:  Iran yaapa kulipiza kisasi baada ya shambulizi kubwa tangu mapinduzi ya mwaka 1979

Wakati Walebanon wakikabiliana wenyewe kwa wenyewe, vikosi vya Israel vilivamia kusini mwa Lebanon mnamo 1978 na mwaka 1982 ili kuwafurusha wapiganaji wa Palestina waliokuwa wakilitumia eneo hilo kama kituo cha kupanga mikakati ya kuishambulia Israel.

Beirut, Lebanon | Waombolezaji wakusanyika wakati wa mazishi ya naibu mkuu wa kundi la Hamas Saleh al-Arouri
Waombolezaji wakusanyika wakati wa mazishi ya naibu mkuu wa kundi la Hamas Saleh al-ArouriPicha: Mohamed Azakir/REUTERS

Baadaye, kundi la Waislamu wa madhehebu ya Shia waliamua kupambana na majeshi ya Israel. Nayo Iran kwa kuzingatia fursa ya kujijengea ushawishi katika ulimwengu wa Kiarabu, ilianza kutoa mafunzo na kuwafadhili wanamgambo hao wapya.

Iran imekuwa ikifadhili makundi kadhaa huko Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Hamas, Hezbollah na makundi mengine ya wanamgambo nchini Iraq. Hivi karibuni, serikali ya Marekani ilikadiria kuwa Iran inatoa ufadhili wa kiasi cha dola milioni 700 kila mwaka kwa kundi la Hezbollah.

Ni zipi sera za Hezbollah?

Mnamo mwaka 1985, Hezbollah ilitoa ilani ambayo iliorodhesha idadi ya malengo yake ikiwa ni pamoja na kuyaondoa mataifa ya kikoloni ya Magharibi nchini Lebanon, kuisambaratisha dola ya Israel na utiifu kwa Iran.

Sehemu ya sera ya awali ya Hezbollah ilikuwa ikitoa pia wito wa kuwepo utawala wa Kiislamu nchini Lebanon kwa kuzingatia mtindo wa kidini wa Iran.

Lakini, baada ya muda kadhaa, malengo ya ndani ya Hezbollah kwa kiasi fulani yalipunguza makali kwani kundi hilo lilianza kujihusisha zaidi na harakati za kisiasa.

Mnamo mwaka wa 2009, Hezbollah ilichapisha ilani mpya iliyokiri kwamba uwepo wa serikali ya Kiislamu haufai kwa nchi ya Lebanon.