1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Kesi ya kihistoria dhidi ya Trump yaanza New York

16 Aprili 2024

Kesi ya kwanza ya uhalifu kuwahi kufunguliwa dhidi ya rais wa zamani nchini Marekani imeanza mjini New York na kumfanya mshitakiwa Donald Trump kufika mahakamani kuhudhuria vikao vya kwanza vya kesi hiyo ya kihistoria.

https://p.dw.com/p/4ep9K
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump
Trump ndiye rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kuwahi kushitakiwa kwa uhalifuPicha: Angela Weiss/REUTERS

Kikao kilianza kwa mchakato mgumu wa kuteuwa jopo la watoa uamuzi wa mahakama la kusikiliza mashitaka yanayomkabili rais huyo wa zamani kwa kughushi rekodi za biashara katika mpango wake wa kuficha madai ya ngono na mwigizaji wa filamu Stormy Daniels.

Siku ilikamilika bila kuchaguliwa wanachama wowote wa jopo hilo la mahakama. Mchakato wa uteuzi wa wanachama 12 wa jopo hilo la watoa uamuzi wa mahakama utaendelea Jumanne.

Soma pia: Donald Trump na msururu wake wa mashtaka mahakamani

Zaidi ya watu 50 walijiondoa katika mchakato huo wa uteuzi wakisema hawawezi kuwa waadilifu na bila ya upendeleo kwa rais huyo wa zamani mwenye utata.

Kesi hiyo huenda ikamuweka Trump mahakamani kwa wiki kadhaa na kuvuruga jaribio lake la kurejea katika Ikulu ya White House. Anatarajiwa kuhudhuria vikao vya mahakama ya Manhattan siku nne kwa wiki. Jaji Juan Merchan ndiye anayeongoza kesi hiyo.