1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaiduwaza Tanzania katika Afcon

Bruce Amani
28 Juni 2019

Michael Olunga alifunga mara mbili wakati Kenya iliwabwaga majirani zake Tanzania kwa mabao 3 – 2 mjini Cairo na kuyaweka hai matumaini ya kutinga duru ya pili ya Kombe la Mataifa ya Afrika

https://p.dw.com/p/3LDEk
Afrika-Cup 2019 Kenia - Tansania
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

Mshambuliaji huyo anayecheza kandanda la kulipowa nchini Japan alisawazisha katika kipindi cha kwanza na akafunga bao la ushindi katika dakika ya 80 ya mtanange huo wa kusisimua ambao ulikuwa ni debi ya Afrika Mashariki.

Johanna Omolo alikuwa mfungaji mwingine wa Kenya, ambayo ilijikuta nyuma 2 – 1 katika kipindi cha kwanza. Saimon Msuva na Mbwana Samatta waliifungia Tanzania, ambao hawajawahi kushinda mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika tangu waliposhiriki mara mbili miaka 39 iliyopita.

Awali, Algeria iliifunga Senegal 1 – 0 katika mechi ya Kundi C iliyokumbwa na matukio ya kuchezeana ngware na nchi zote mbili zinatarajiwa kutinga hatua ya 16 za mwisho.

Hata kama Kenya ikipoteza mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Senegal, watatumai kupenya katika hatua ya mtoano kama mojawapo ya timu bora nne zitakazomaliza katika nafasi ya tatu kwenye makundi.

Baada ya mechi mbili, mabingwa wa zamani Algeria wana pointi sita, Senegal na Kenya wana tatu kila mmoja na Tanzania hawana chochote. Mechi kati ya Kenya na Senegal itaamua nani atamaliza katika nafasi mbili za kwanza pamoja na Algeria katika kundi hilo.

Makocha wote wawili Sebastian Migne wa Kenya na Emmanuel Amunike wa Tanzania wameelezea mechi hiyo kuwa ya vituko.

Mfaransa Migne alizungumza kabla ya mechi kuhusu umuhimu wa timu yake kuanza vyema lakini Tanzania ndio timu iliyojituma zaidi katika dakika za mapema na kuchukua usukani baada ya dakika sita pekee. Kipa wa Kenya Patrick Matasi alipangua shuti ya nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta na Msuva akamalizia

Stars walijaribu kusawazisha huku mipira ya kichwa ya Francis Kahata na Olunga ikigonga besela.

Kisha kipa wa Tanzania Aishi Manula akashindwa kuuondoa kwa ngumi mpira wa freekick, ukamgonga mwenzake Erasto Nyoni na ukaelekea kwa Olunga, ambaye alipiga mkasi hadi wavuni.

Sherehe za Kenya zilizimwa mara moja baada ya Samatta kuwaadhibu mabeki wa kenya na kusukuma wavuni kombora kuiweka Tanzania kifua mbele 2 – 1 katika kipindi cha kwanza. Manula alifanya kazi akapangua mpira wa kichwa uliopigwa na Wanyama. Lakini kipa huyo hangeweza kuizuia Kenya kusawazisha kwa mara ya pili katika dakika y a62 wakati krosi safi kutokana na kona fupi ilisukumwa wavuni kupitia kichwa cha Johanna Omolo.

Mambo yaliwaharibikia Tanzania dakika 10 kabla ya mechi kuisha, kwa kujikuta nyuma kwa mara ya kwanza katika mechi hiyo wakato Olunga alisukuma kambani bao la tatu.

Akizungumza baada ya mechi, kocha wa Harambee Stars Migne amesema wachezaji wake wameandika historia, na sasa kila kitu kinawezekana, kwa sababu hawana chochote cha kupoteza.

Mwenzake wa Taifa Stars Amunike aliikosoa timu yake. Alisema kulikuwa vituko vingi, wachezaji walifanya makosa mengi licha kuwa walifanya mazoezi makali na kujiandaa kwa mchuano huo.

Ijapokuwa timu zote mbili sio miamba wa kandanda la Afrika, zilionyesha mchezo mzuri wenye nafasi kadhaa za wazi za kufunga mabao.

Katika mechi ya awali, Madagascar iliichapa Burundi 1 – 0, na kuwaweka wageni wa tamasha la mwaka huu Madagascar katika ukingo wa kufuzu katika hatua ya 16  za mwisho kutoka Kundi B. Madagascar ilishinda baada ya Marco Ilaimaharita kusukuma wavuni freekick safi sana kutoka nje ya eneo la hatari.

Wageni hao wanahitaji sasa kutoka sare dhidi ya Nigeria ili kuwa na uhakika wa kupenya, au Guinea ishindwe kuishinda Burundi. Madagascar inaweza pia kufuzu kama mojawapo ya timu bora za nafasi ya tatu kwenye makundi.