1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waathirika mashambulizi ya ubalozi wa Marekani hawajafidiwa

Mohammed Khelef
7 Agosti 2023

Baraza la Seneti nchini Kenya limeingilia kati baada ya kubainika kuwa waathirika wa mashambulizi ya kigaidi kwenye ubalozi wa Marekani jijini Nairobi miaka 25 iliyopita bado hawajapata fidia hadi sasa.

https://p.dw.com/p/4UrGb
Kenia | Explosionen in der US-Botschaft, Überlebende
Picha: DW

Imepita miaka 25 tangu shambulio la bomu la ubalozi wa Marekani jijini Nairobi kusababisha maafa na kuacha majeruhi.

Waathiriwa hao bado wanasaka fidia kutoka kwa serikali ya Marekani.

Soma zaidi: Miaka 20 baada ya mashambulizi ya pamoja Kenya na Tanzania, Ugaidi bado ni kitisho

Douglas Sidialo ni mmoja ya waliojeruhiwa kwenye shambulio hilo la kigaidi la mwaka 1998, naye anasema maisha yake yalibadilika na alipoteza uwezo wake wa kuona.

"Kwa sasa nahitaji usaidizi kufanya shughuli za kila siku." Anasema manusura huyo.  

Seneti yaingilia kati

Ili kuiongeza kasi ya kudai fidia kutoka kwa serikali ya Marekani, Kamati ya Muda ya Seneti ilianzisha mchakato mpya. Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati hiyo, Agnes Kavindu, anasema "upo mpango wa kukutana na baraza la Seneti la Marekani ili kufuatilia suala la fidia."

Kenia Nairobi Gewalt bei Protesten gegen Regierung
Afisa wa usalama wa Kenya.Picha: THOMAS MUKOYA/REUTERS

Kamati hiyo ya muda ilikuwa inatarajiwa kuhudhuria hafla ya kumbukumbu ya 25 ya mkasa huo jijini Nairobi.

Soma zaidi: Kesi ya Ghailani yaanza, Marekani.

Itakumbukwa kuwa lori lililosheheni mabomu liliripuka nje ya ubalozi wa Marekani uliokuwa katikati ya jiji la Nairobi na shambulio jengine lilitokea Dar es Salaam katika nchi jirani ya Tanzania kwa wakati mmoja. 

Marekani ilimtuhumu kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Qaeda, Osama Bin Laden aliyeuawa mwaka 2011, kwa kuamuru na kupanga mashambulizi hayo.

Marekani kutowa kauli

Siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Anthony Blinken, alikuwa anatazamiwa kutoa taarifa maalum ya kumbukumbu ya miaka 25 tangu shambulio hilo kutokea.

US-Außenminister Blinken in Australien
Waziri wa Mambo wa Kigeni wa Marekani, Antony Blinken.Picha: Darren England/AAP/dpa

Hafla hiyo ilitarajiwa kurushwa mubashara mtandaoni kutokea Marekani

Soma zaidi: Sheria ya ugaidi yazusha upinzani tena Kenya

Tangu shambulzi hilo, ubalozi wa Marekani ulihamishiwa Mtaa wa Gigiri mkabala na makao makuu ya Umoja wa Mataifa nje kidogo ya Jiji la Nairobi.

Bustani ya kumbukumbu ilianzishwa ulipokuwa ubalozi huo katikati ya jiji. 

Imetayarishwa na Thelma Mwadzaya/DW Nairobi