1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni zaanza katika uchaguzi muhimu DRC

22 Novemba 2018

Baada ya miaka miwili ya kurudi nyuma, ahadi zisizotimia na ucheleweshaji, hatimaye Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imefungua milango ya kampeni za uchaguzi muhimu ambao unaweza kuamua hatma ya taifa hilo.

https://p.dw.com/p/38hvI
Kongo Emmanuel Ramazani Shadary
Picha: REUTERS

Wapigakura watachagua hapo Desemba 23, mrithi wa rais anaemaliza muda wake Joseph Kabila, ambae amesalia madarakani kikatiba kama kiongozi msimamizi hata baada ya kukamilika muhula wake wa pili na wa mwisho miaka miwili iliyopita.

Suala muhimu katika uchaguzi huu ni uongozi wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini ambalo halijawahi kushuhudia makabidhiano ya amani ya madaraka tangu lilipopata uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

Upande wa mashariki mwa Congo umeharibiwa na miongo kadhaa ya umuagaji damu wa kikabilia na machafuko yanayosababishwa na wanamgambo, pamoja na mripuko mbaya wa ugonjwa wa Ebola, vinavyoupa changamoto ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa ulioko nchini humo.

Demokratische Republik Kongo Wahlmaschine
Mjumbe wa tume ya uchaguzi Jean-Pierre Kalamba akionesha orodha za wagombea wa nafasi mbalimbali za uchaguzi, wakati wa uwasilishaji mada juu ya mashine za kupigia kura, Februari 21, 2018.Picha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Shadary chini ya vikwazo vya EU

Wagombea 21 wameandikishwa kuwania nafasi ya kumrithi Kabila mwenye umri wa miaka 47, ambae ameitawala nchi hiyo tangu Januari 2001, baada ya kuuawa kwa baba yake Laurent-Desire Kabila. Karibu nusu ya raia wa Congo milioni 80 wana haki ya kupiga kura.

Baada ya kukabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa dhidi ya kuwania muhula wa tatu, Kabila aliamua kumuunga mkono mteule wake Emmanuel Ramazani Shadary mwezi Agosti.

Shadary ni mmoja ya Wacongo 15 waliowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya, wakituhumiwa kwa uvunjaji wa haki za binadamu wakati alipokuwa waziri wa mambo ya ndani kati ya Desemba 2016 na mwanazoni mwa 2018.

Mmoja ya wapinzani wakuu wa Shadary ni Martin Fayulu, mbunge asiejulikana ambaye mapema mwezi huu aliteuliwa kuwa mgombea wa pamoja wa vyama kadhaa vya upinzani -- lakini siyo vyote -- vinavyounda muungano bungeni.

Wapiga kampeni wa Shadary wauawa Kasai

Katika ishara ya uwezekano wa kuzuka vurugu za uchaguzi, wanaharakati watatu wa kisiasa wanaomtafutia kura Shadary wameuawa katika mkoa wenye machafuko wa Kasai, walisema wanafamilia siku ya Jumatano.

DR Kongo Martin Fayulu
Mgombea wa upinzani Martin Fayulu.Picha: Getty Images/AFP/T. Charlier

Tume ya uchaguzi CENI inasimamia uamuzi wake wa kutumia mashine 106,000 za kielektoniki katika uchaguzi huo, zilizotolea na Korea Kusini, licha ya matakwa ya upinzani -- na hasa Fayulu-- ya kutumia karatasi.

"Ni ujumbe huo huo kama Wacongo wanaotaka uchaguzi mzuri Desemba 23. Uchaguzi bila mashine za kupigia kura, uchaguzi ulio na orodha iliosahihishwa ya wapigakura," alisema Adolphe Muzito, kiongozi mwingine wa upinzani wa kisiasa.

Serikali ya Congo ambayo ina uhusiano mgumu na Umoja wa Mataifa, imekataa aina yoyote ya msaada wa kimataifa wakifedha au wa vifaa kwa ajili ya uchaguzi katika taifa hilo la pili kwa ukubwa barani Afrika.

Ujumbe wa kulinda amani wa MONUSCO umependekeza kutumia helikopta zake na ndege kusafirisha mashine za kupigia kura nchini kote. Lakini serikali mjini Kinshasa inataka ujumbe huo uondoke kufikia 2020.

Katika mji wa Beni ulioko mashariki kwenye mpaka na Uganda ambao umeshuhudia migogoro mibaya zaidi nchini DRC na pia madhara ya mripuko wa Ebola, wakazi wameelezea matumaini kwamba uchaguzi huu utaleta mabadiliko katika maisha yao.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,afpetv.

Mhariri: Saumu Yusuf