Jeshi la Ukraine lafanyiwa mabadiliko | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Jeshi la Ukraine lafanyiwa mabadiliko

Serikali ya Ukraine imefanya mabadiliko katika uongozi wa jeshi la nchi hiyo huku machafuko yakizidi mashariki mwa nchi hiyo licha ya shinikizo kuzidi kutoka kwa Marekani na Ujerumani dhidi ya Urusi

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine amemteua waziri mpya wa ulinzi na mkuu mpya wa majeshi huku vikosi vya wanajeshi wa serikali vikiendelea kufanya operesheni mashariki mwa Ukraine kujaribu kumaliza uasi katika eneo hilo lenye shughuli nyingi za kiviwanda.

Punde tu baada ya kuteuliwa, Waziri mpya wa ulinzi, Valeriy Geletey, ameahidi kukabiliana vikali na waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki siku chache tu baada ya Rais Poroshenko kukataa kuurefusha muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Majeshi yaongeza mashambulizi

Majeshi ya Ukraine yakiwa na vifaru na ndege za kivita yameongeza operesheni za kijeshi tangu kumalizika kwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano. Lakini majeshi hayo ambayo hayana mafunzo ya hali ya juu na hayana vifaa vya kutosha yanakabiliwa na mtihani mkubwa katika kukabiliana na waasi ambao wanaonekana kujihami vilivyo na ambao wanadaiwa kupewa silaha na kufadhiliwa na Urusi, madai ambayo Urusi imeyakanusha.

Wanajeshi wa Ukraine wakishika doria mjini Slovyansk

Wanajeshi wa Ukraine wakishika doria mjini Slovyansk

Idara ya ulinzi wa mipakani imesema wanajeshi tisa wamejeruhiwa hii leo baada ya makombora kurushwa katika eneo la mpakani kati ya Urusi na Ukraine na washambuliaji wamewaua askari watatu na kumjeruhi mwingine katika mji wa Donetsk, huku waasi 150 wakiripotiwa kuuawa.

Mkaazi mmoja wa mji wa Kramatorska pia ameuawa katika mashambulizi ya waasi ambayo yamewalazimu wafanyakazi wa viwandani kuwataka wasimamizi wao kusitisha operesheni katika viwanda.

Ghasia hizo zinakuja licha ya juhudi kabambe za kidiplomasia za kujaribu kuzishawishi pande zote mbili zinazozozana kukubali kufanya duru mpya ya mazungumzo ya kutafuta makubaliano mapya ya kusitisha mapigano.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wamemuomba Rais Vladimir Putin wa Urusi kwa njia ya simu kusaidia katika kuandaa mkutano mwingine wa wajumbe wa pande hizo mbili ifikapo mwishoni mwa wiki hii.

Urusi yatakiwa kuupunguza mzozo

Ofisi ya Merkel imesema Kansela huyo amezungumza pia na Rais Barrack Obama wa Marekani kwa njia ya simu ambapo wamesema wamemuhimiza Putin kuwepo haja ya kusitisha haraka mapigano ambayo yataheshimiwa na pande zote mbili.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,Rais wa Ukraine Petro Poroshenko na Rais wa Urusi Vladimir Putin

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,Rais wa Ukraine Petro Poroshenko na Rais wa Urusi Vladimir Putin

Ikulu ya rais wa Marekani imesema Obama na Merkel wamekubaliana kuwa iwapo Urusi haitaupunguza mzozo wa mashariki mwa Ukraine katika kipindi kifupi kijacho, basi Marekani na Umoja wa Ulaya watashirikiana kuiwekea Urusi vikwazo zaidi.

Kufikia sasa, Putin amekataa kuwataka waasi hao wa mashariki mwa Ukraine kusitisha mapigano na badala yake anamlaumu Poroshenko kwa kushindwa kutekelezwa kwa makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano.

Katika ujumbe wa kheri aliomtumia Obama hii leo katika kusherehekea siku ya uhuru wa Marekani, Putin amesema Urusi na Marekani zote zina wajibu wa kuhakikisha amani na uthibiti duniani na zinapaswa kushirikiana zaidi kwa maslahi sio tu ya nchi zao bali za dunia nzima kwa jumla.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com