1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je nchi za Ghuba zitaunda mfungamano kama wa NATO?

Zainab Aziz / Cathrin Schaer
24 Septemba 2025

Qatar ilishambuliwa na Israel hivi karibuni ikiwalenga viongozi wa Hamas waliokuwa wanakutana Doha kujadili uwezekano wa kusimamisha mapigano Gaza. Kati ya waliouwawa walikuwemo pia Waqatari.

https://p.dw.com/p/510v1
Wajumbe kutoka nchi sita za Baraza la Ushirikiano wa eneo la Ghuba, GCC,
Je nchi za Ghuba zitaunda mfungamano wa kujihami kama ule wa NATO?Picha: Amiri Diwan/Anadolu/picture alliance

Baada ya mashambulio yaliyofanywa na Israel nchini Qatar, viongozi wa nchi za Ghuba sasa wanasonga mbele na juhudi za kuziwezesha nchi zao kujitegemea zenyewe kiulinzi ili kuondokana na sera ya kuitegemea Marekani.

Hayo ameeleza mkurugenzi wa kitengo cha masuala ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kwenye taasisi ya Chatham, Sanam Vakil. Amesema mnamo siku za hivi karibuni pamekuwapo harakati na mazungumzo juu ya lengo la kuunda jumuiya ya kijeshi miongoni mwa nchi za kiarabu mithili ya ile ya  NATO.

Wiki iliyopita viongozi wa nchi za kiarabu waliitisha mkutano wa dharura ulioandaliwa na jumuiya ya Umoja wa nchi za kiarabu pamoja na shirika la Ushirikiano la nchi za Kiislamu.

Wajumbe wa Misri walipendekeza kuwepo kwa kikosi kazi cha pamoja cha mataifa ya Kiarabu katika muundo kama wa NATO. Katika hotuba yake kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia al-Sudani, pia alitoa wito wa kuwepo kwa mtazamo wa pamoja juu ya usalama wa nchi za kiarabu.

Wajumbe kutoka nchi sita za Baraza la Ushirikiano wa eneo la Ghuba, GCC, wamesema wataweka ibara katika makubaliano juu ya ulinzi wa pamoja. Kwa mujibu wa ibara hiyo, mwanachama mmoja akishambuliwa basi wote wengine  wameshambuliwa. Makubaliano ya ulinzi ya nchi hizo yalitiwa saini kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000.

Kwanini Israel inayashambulia majengo Gaza City?

Nchi hizo za shirika la GCC ni Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu. Utaratibu huo ni sawa na ule wa jumuiya ya kijeshi ya NATO kwa mujibu wa ibara ya 5 ya mkataba wa mfungamano huo wa kijeshi.

Baada ya mkutano wa dharura, mawaziri wa ulinzi wa nchi za Ghuba walikutana tena mjini Doha na kukubaliana juu ya kuweka utaratibu wa pamoja wa taarifa za kijasusi. Nchi hizo pia zilitangaza mipango ya kufanya mazoezi ya kijeshi ya pamoja. Na mnamo wiki hiyo hiyo Suadi Arabia ilitangaza kuingia katika makubaliano ya ulinzi na Pakistan. Nchi hizo zimekubaliana kulindana, yaani mmoja akishambuliwa ndio sawa na mwengine pia ameshambuliwa.

Hata hivyo wadadisi wana mashaka iwapo itawezekana kwa nchi za kiarabu kujenga mfungamano wa kijeshi ili kuweza kujihami dhidi ya Israel. Wanasema hakuna nchi ya Ghuba inayotaka uhasama na Israel licha ya ukweli kwamba hali imebadilika baada ya Israel kuishambulia Qatar.

Wadadisi wanaamini nchi za kiarabu zitaweka utaratibu tofauti na ule wa NATO. Wanaamini kwamba huenda nchi sita za Ghuba zikajenga mahusiano ya kiulinzi na Uturuki pamoja na Misri. Uhusiano huo ni jambo linalowezekana tukitilia maanani kwamba Uturuki imeweka majeshi yake nchini Qatar tangu mwaka 2017.