1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je makubaliano ya kusitisha mapigano Yemen yatafanikiwa?

Lilian Mtono
5 Aprili 2022

Makubaliano ya amani ya miezi miwili yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa yalianza kutekelezwa nchini Yemen Jumamosi. Wachambuzi wanatumai kuwepo kwa utulivu katika vita vilivyodumu miaka saba katika nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/49T8j
Jemen Huthi-Rebellen in Sanaa
Picha: imago images/Xinhua

Waasi wa Kihuthi wanaoungwa mkono na Iran na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao uliingilia kati mwaka wa 2015 ili kuiokoa serikali ya Yemen dhidi ya waasi hao mwaka mmoja baada ya kuuteka mji mkuu wa Sanaa, wote wamekubaliana kuzingatia usitishaji huo wa mapigano. Lakini makubaliano hayo yatafanikiwa wakati mawili yaliotiwa saini hapo awali yamesambaratika?

Mohammed Al-Basha, mtaalam wa Yemen wa shirika la utafiti la Navanti lenye makao yake nchini Marekani, anasema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kuvurugwa usambazaji wa chakula na nishati duniani ni kichochezi cha kuwepo na makubaliano hayo. Al-Basha anasema uhasama wa muda mrefu nchini Ukraine unaleta udharura wa kumaliza vita nchini Yemen.

Vita vya Yemen vimewauwa mamia kwa maelfu moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kusababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao, pamoja na mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani, kulingana na Umoja wa Mataifa. Angalau asilimia 80 ya watu milioni 30 nchini humo wanategemea misaada kutoka nje.

Jemen Saada Zerstörung Gefängnis durch Luftangriff
Jengo lililoharibiwa katika mji wa Saada huko YemenPicha: Ansarullah media center/AFP

Ahmed Nagi wa Kituo cha utafiti kuhusu Mashariki ya Kati cha Malcom H. Kerr Carnegie huko Beirut anasema huku mapigano yakiwa yamekwama, mapatano yamekuwa ya lazima na Wahuthi wanahisi hawawezi tena kuendelea na uhasama baada ya vita vya Shabwa na Marib, na hasara ya kifedha waliyoipata.

Vikosi vinavyoiunga mkono serikali vilitwaa udhibiti wa eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Shabwa kusini mwa Yemen mapema mwaka huu.

Wakati huo huo Wahuthi wamejaribu kwa miezi kadhaa kusonga mbele katika eneo jirani la Marib, ambalo mji mkuu wake ni ngome ya mwisho ya serikali kaskazini mwa nchi.

Kulingana na Nagi, muungano unaoongozwa na Saudi Arabiaunaamini kwamba kuendelea kwa vita kutasaidia tu kupanua athari zake kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu,wahusika wawili wakuu katika muungano huo.

Katika mwaka uliopita,wapiganaji wa Huthi wameanzisha mfululizo wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, na kuathiri miundombinu muhimu. Mwezi uliopita, walishambulia maeneo 16 nchini Saudi Arabia, na kusababisha moto mkali kwenye kiwanda cha mafuta karibu na mji wa Jeddah.

BG Protest in der jemenitischen Hauptstadt Sanaa gegen die anhaltende Treibstoffkrise
Maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya vyakula YemenPicha: Mohammed Hamoud/AA/picture alliance

Saudi Arabia imeonya kwamba mashambulizi kama hayo kwenye vituo vyake vya mafuta yanaweza kuharibu uwezo wa ufalme huo kukidhi mahitaji ghafi ya kimataifa kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Makubaliano hayo yanayokaribishwa na mataifa yenye nguvu duniani yanaweza kurefushwa zaidi ya miezi miwili ikiwa pande zote mbili zitaridhia. Ilikuja baada ya juhudi kubwa za kidiplomasia, ikiwa ni pamoja na mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea nchini Saudi Arabia ambayo waasi waliyapuuza kwa sababu yaliandaliwa na kile walichodai kuwa ni adui wao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema anatumai mapatano hayo yatasababisha mchakato wa kisiasa utakaoleta amani nchini Yemen. Kwa upande wake,Rais wa Marekani Joe Biden alisisitiza kuwa ni muhimu kumaliza vita hivi. Mtafiti Nagi alisema mapatano hayo yanaweza kutumika kama msingi wa kupatikana kwa suluhu ya kisiasa.