1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Yemen vyasababisha zaidi vifo vya watoto-UNICEF

Saumu Mwasimba
12 Machi 2022

Takriban watoto 46 waliuwawa au kujeruhiwa kwenye vita nchini Yemen katika kipindi cha miezi miwili ya mwaka wa mwaka 2022 wakati mapigano yakiongezeka

https://p.dw.com/p/48OOx
BG Jemen Corona Pandemie medizinische Versorgung
Picha: Abdulnasser Alseddik/AA/picture alliance

Takriban watoto 46 waliuwawa au kujeruhiwa kwenye vita nchini Yemen katika kipindi cha miezi miwili ya mwaka wa mwaka 2022 wakati mapigano yakiongezeka kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Kihouthi.

Hayo yameelezwa na afisa wa Umoja wa Mataifa Jumamosi,Phillippe Duamelle. Mwakilishi huyo wa shirika la kuhudumia watoto la UN nchini Yemen,amesema vita vimeendelea kuongezeka mwaka huu na kama ilivyo kila wakati watoto ndio wahanga wa mwanzo na wanaopata madhara zaidi.

BG Jemen Corona Pandemie medizinische Versorgung
Picha: Abdulnasser Alseddik/AA/picture alliance

Yemen inakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe  tangu mwaka 2014 baada ya waasi wakihouthi kuudhibiti mji mkuu Sanaa na sehemu kubwa ya nchi hiyo upande wa Kaskazini,na serikali ikalazimika kukimbilia upande wa Kusini  na kisha Saudi Arabia.

 Muungano wa kijeshi unaopambana na waasi hao,ukiongozwa na Saudi Arabia uliingia YemenMachi 2015 ukiungwa mkono na Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu kujaribu kumrudisha madarakani rais Abed Rabbo Mansour Hadi.

BG Protest in der jemenitischen Hauptstadt Sanaa gegen die anhaltende Treibstoffkrise
Picha: Mohammed Hamoud/AA/picture alliance

Vita hivyo vimeongezeka tangu mwanzoni mwa 2022 wakati muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia ulipojiimarisha na kuongeza hatua ya kuvisaidia vikosi  vya kijeshi vya ardhini vya  serikali  ya Yemen kukabiliana na mashambulizi ya wahouthi katika mji wa Marib.

Mapigano yameongezeka pia katika sehemu nyingine za nchi hiyo ya kiarabu masikini kabisa duniani. Mwakilishi wa UNICEF Duamelle amesema vita hivyo vimesababisha watoto 10,200 kupoteza maisha au kujeruhiwa  katika kipindi cha miaka miaka 7 na idadi kamili inawezekana kuwa kubwa zaidi.

Aidha ni vita vilivyosababisha pia mgogoro mbaya  kabisa  wa kibinadamu duniani.