1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je hukumu ya Ongwen itatoa haki kwa wahanga wa mateso?

Grace Kabogo
4 Februari 2021

Kamanda wa zamani wa kundi la waasi wa Lords Resistance Army nchini Uganda, LRA Dominic Ongwen amekutwa na hatia ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu

https://p.dw.com/p/3ot35
Niederlande Dominic Ongwen vor dem  Internationalen Strafgerichtshof
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Dejong

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC imemkuta Ongwen na hatia ya makosa 61 kati ya 70 ya uhalifu ikiwemo mauaji, ubakaji, utumwa wa ngono, ndoa za kulazimisha, utekaji nyara watoto na kuwaandikisha kama wapiganaji, utesaji na mauaji. Akiisoma hukumu hiyo mjini The Hague, Jaji Bertram Schmitt amesema Ongwen, mwenye umri wa miaka 46, ambaye alitekwa nyara na waasi akiwa mtoto wa miaka tisa na kuingizwa katika jeshi la waasi wa LRA na baadae kuwa kamanda wa waasi, alifanya uhalifu huo kwa hiari yake kati ya mwaka wa 2002 na 2005.

''Dominic Ongwen amekutwa na hatia bila ya kuwa na mashaka yoyote ya uhalifu kadhaa, katika muktadha wa mashambulizi manne maalum kwenye kambi za wakimbizi wa ndani za Pajula, Odek, Lukudi na Abok. Hatia ya mashambulizi dhidi ya raia, mauaji, jaribio la mauaji, utumwa, uporaji, uharibifu wa mali pamoja na utesaji", alisema jaji Schmitt.

Majaji wa mahakama ya ICC walikataa utetezi uliotolewa kwamba Ongwen mwenyewe ni muhanga, kutokana na kutekwa nyara akiwa mtoto na aliathirika kisaikolojia. Hata hivyo, Jaji Schmitt amesema mahakama hiyo inafahamu kuwa Ongwen aliteseka, lakini kesi hiyo ni kuhusu uhalifu uliofanywa na Ongwen akiwa mtu mzima na kamanda wa LRA, hivyo lazima awajibishwe.

Dominic Ongwen Gerichtsprozess 26.01.2015 Den Haag
Dominic OngwenPicha: picture-alliance/epa/P. Dejong

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, limesema kesi hiyo ilikuwa ya kihistoria katika kufanikisha haki ya wahanga wa mateso yaliyofanywa na waasi wa LRA. Mkurugenzi mwenza wa mpango wa haki ya kimataifa ya shirika hilo, Elise Keppler amesema kesi hii ni hatua muhimu kama kesi ya kwanza na ya pekee kwa mpiganaji wa LRA kufikishwa ICC na uamuzi kutolewa.

ICC yasikiliza kesi ya Dominic Ongwen wa kundi la LRA

Nalo shirika la haki za binaadamu la Amnesty International limesema linaamini kuwa uamuzi wa ICC utatoa haki ya muda mrefu kwa waathirika ambao bado hawajapata haki ya madhila waliyopitia. Adhabu dhidi ya Ongwen itatangazwa baadae.

Kundi la LRA lilianzishwa miongo mitatu iliyopita na Joseph Kony, aliyeanzisha uasi kaskazini mwa Uganda dhidi ya utawala wa Rais Yoweri Museveni. Umoja wa Mataifa umesema waasi wa LRA wamewaua zaidi ya watu 100,000 na kuwateka nyara watoto 60,000 katika ghasia ambazo zilisambaa kwenye mataifa mengine matatu ya Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Ongwen alijisalimisha kwa vikosi maalum vya Marekani vilivyokuwa vinamtafuta Kony katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mwanzoni mwa mwaka 2015 na kupelekwa ICC.