1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Itachukuwa miaka 16, dola bilioni 40 kuijenga tena Gaza - UM

2 Mei 2024

Umoja wa Mataifa unakisia kwamba itagharimu hadi dola bilioni 40 na miaka 16 kuweza kuurejesha Ukanda wa Gaza kwenye hali ya kawaida baada ya uharibifu mkubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu Vita vya Pili vya Dunia.

https://p.dw.com/p/4fR8J
Ukanda wa Gaza
Umoja wa Mataifa unakisia kwamba itagharimu hadi dola bilioni 40 na miaka 16 kuweza kuujenga tena Ukanda wa Gaza.Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Abdallah al-Dardari, alisema siku ya Alkhamis (Mei 2) kwamba makisio ya awali ya Mfuko Maendeleo wa Umoja huo yalikuwa yanaonesha kwamba ujezi mpya wa Gaza utapindukia dola bilioni 30 na kwamba unaweza kufikia hadi dola bilioni 40.

"Kiwango cha uharibifu ni kikubwa mno na kisichokadirika. Hii ni hali ambayo jamii ya kilimwengu haijawahi kukabiliana nayo tangu Vita vya Pili vya Dunia." Alisema Dardari.

Umoja wa Mataifa unakisia kuwa hata kama vita kwenye Ukanda wa Gaza vitamalizika leo, basi itachukuwa miaka 16 kutoka sasa kuweza kuyajenga tena majengo yote yaliyoharibiwa ndani ya kipindi cha miezi saba tu cha mashambulizi ya Israel.

Soma zaidi: Vita vya Gaza: Blinken akutana na Netanyahu

Kauli ya msaidizi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inaashiria hali halisi cha madhara ambayo yameikumba Gaza tangu Israel ilipoanzisha operesheni yake ya kijeshi kufuatia mashambulizi ya wanamgambo wa Kipalestina ya tarehe 7 Oktoba, ambapo walilivamia eneo la kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya watu wapatao 1,200 na kuwachukuwa mateka wengine wapatao 250.

Tangu hapo, Israel imekuwa ikitumia silaha nzito nzito kuteketeza majengo ya aina mbalimbali ndani ya Ukanda wa Gaza, yakiwemo makaazi ya watu, hospitali, skuli, masoko, misikiti na makanisa. 

Hamas yaelekea kukubali usitishaji mapigano

Kundi la Hamas lilisema siku ya Alkhamis kwamba lingetuma ujumbe wake mjini Kairo haraka iwezekanavyo ili kuendelea na mazungumzo ya kusitisha mapigano, kujibu pendekezo la hivi karibuni la Misri.

Kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas, Ismail Haniyeh.
Kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas, Ismail Haniyeh.Picha: Fazil Abd Erahim/AA/picture alliance

Kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo, Ismail Haniyeh, alisema tayari alishazungumza na mkuu wa idara ya ujasusi ya Misri na kusisitiza "muelekeo chanya kwenye kulisoma pendekezo hilo la kusitisha mapigano."

Soma zaidi: Netanyahu asema Israel itajiamulia yenyewe masuala yake ya usalama

Kwenye ziara ya siku ya Jumatano (Mei 1) nchini Israel, ambayo ilikuwa ya saba tangu vita hivyo kuanza, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, alishinikiza kufikiwa kwa makubaliano hayo. 

Pendekezo la mkataba wa kusitisha mapigano linataka kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel walio mikononi mwa Hamas, ambapo nayo Israel itasitisha mashambulizi yake na kufikisha chakula, madawa na maji kwa watu wa Gaza. 

Vile vile, Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Israel nao pia wanatazamiwa kuwa sehemu ya makubaliano hayo.

Marekani, mshirika mkubwa waIsrael, imekuwa ikiushinikiza utawala wa Benjamin Netanyahu kuongeza idadi na kasi ya ufikishaji misaada kwa raia wenye mahitaji makubwa ndani ya Gaza, na hapo jana Israel iliufunguwa tena mpaka wa kaskazini mwa ukanda huo kwa mara ya kwanza tangu ulipofungwa mwanzoni mwa vita.

Vyanzo: AFP, Reuters