1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yamuua kamanda mwandamizi wa Hezbollah

1 Aprili 2026

Israel imetangaza kumuua kamanda mwandamizi wa Hezbollah katika shambulizi la mjini Beirut huku wizara ya afya ya Lebanon ikisema watu saba wameuawa, mnamo wakati Israel ikiendelea kuwalenga viongozi wake.

https://p.dw.com/p/5BWgi
Lebanon Aaramta 2023 | Wapiganaji wa Hezbollah wakati wa mazoezi ya kijeshi kusini mwa Lebanon
Wapiganaji kutoka kundi la wanamgambo wa Lebanon Hezbollah wakifanya mazoezi katika kijiji cha Aaramta katika Wilaya ya Jezzine, kusini mwa Lebanon, 2023.Picha: Hassan Ammar/AP Photo/picture alliance

Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha kiusalama nchini Lebanon pamoja na kingine cha Hezbollah, vilivyozungumza na shirika la habari la AFP, kamanda huyo Youssef Hashem, aliyekuwa akihusika na masuala ya kijeshi ya kundi hilo nchini Iraq, aliuawa ndani ya hema wakati akifanya mkutano.

Jeshi la Israel limesema Hashem alikuwa kamanda wa Hezbollah katika mapambano ya kundi hilo kusini mwa Lebanon. Chanzo kingine kilicho karibu na Hezbollah kilisema Hashem ni "afisa wa ngazi ya juu kulengwa tangu kuanza kwa vita". Mwanachama mwingine wa kundi hilo Mohammad Baqir al-Naboulsi, pia ameuawa katika shambulizi lililofanyika eneo la Jnah mjini Beirut.

Israel pia imesema kuwa inataka kudhibiti tena eneo la kusini karibu na mpaka mwa Lebanon ili kuunda kile ambacho maafisa wamekitaja kama eneo la kiusalama ili kuwafurusha wapiganaji wa Hezbollah. Israel tayari ilikuwa inakalia eneo la kusini mwa Lebanon kwa karibu karne mbili hadi mwaka 2000. Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema Jumanne kwamba nyumba zote katika vijiji vilivyo kando na mpaka zitabomolewa. Lakini waziri mwenzake wa Lebanon Michel Menassa, amelaani mipango hiyo wakati Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney akisema ni "uvamizi usio halali."

Mumbai 2026 | Meli ya mafuta ya LPG Jag Vasant baada ya kupita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz
Meli ya kubeba gesi ya LPG yenye bendera ya India, Jag Vasant, ya kusafirisha gesi ya petroli iliyoyeyushwa, inaonekana katika Bandari ya Mumbai baada ya kuvuka Mlango-Bahari wa Hormuz, Jumatano, Aprili 1, 2026Picha: Rafiq Maqbool/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, mvutano kati ya Marekani na washirika wake wa NATO umeongezeka baada ya Rais Donald Trump kusema kuwa alikuwa akifikiria kuiondoa Marekani kutoka muungano huo wa kijeshi kutokana na wanachama wake wa Ulaya kukataa kutuma meli za kivita kwenda kufungua tena Mlango wa Hormuz.

Naye kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Mojtaba Khamenei ameapa hii leo kuwa nchi yake itaendelea kuunga mkono vikosi vinavyoipinga Israel katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati. Kauli hiyo kutoka kwa Khamenei, kama ilivyo kwa nyingine alizozitoa tangu achaguliwa kuwa kiongozi mkuu, imesomwa tu kupitia vyombo vya habari. Kiongozi huyo hajaonekana hadharani tangu vita vilipoanza  Februari 28 huku maafisa wa Marekani na Israel wakiamini kwamba alijeruhiwa na anaendelea kujificha.

Iran Tehran 2024 | Kiongozi Mkuu mpya wa Iran Mojtaba Khamenei
Kiongozi Mkuu mpya wa Iran Mojtaba Khamenei Picha: Hamed Jafarnejad/ISNA/WANA/REUTERS

Hapo jana kituo cha habari cha  RTVI, kilimnukuu Balozi wa Urusi aliyesema kuwa Khamenei yuko nchini Iran lakini anajizuia kujitokeza hadharani kutokana na "sababu zinazoeleweka". 

Nalo jeshi la Walinzi wa Mapinduzi wa Iran IRGC limesisitiza Jumatano kwamba Mlango Bahari wa Hormuz, utaendelea kufungwa kwa ‘maadui' wa nchi hiyo, huku Rais wa Marekani Donald Trump akisema kwamba atazingatia kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano endapo ungefunguliwa tena.