Israel yadai kunasa nyaraka za siri za Iran | Habari za Ulimwengu | DW | 01.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Israel yadai kunasa nyaraka za siri za Iran

Waziri Mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu amesema ana uthibitisho mpya  kuhusiana na mpango wa silaha za nyukilia wa Iran ambao unaweza kutekelezwa wakati wowote.

 Kwa mujibu wa waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ambaye  hadi wiki iliyopita alikuwa mkurugenzi wa shirika la ujasusi la CIA  nyaraka hizo ni za kweli.  Mara baada ya kurejea kutoka ziara ya Mashariki ya Kati ambako pia alikutana na waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu ,Pompeo amesema taarifa nyingi zilizoko katika makabrasha hayo ni mpya kwa maafisa wa Marekani. 

Amesema nyaraka hizo zilizozinduliwa na waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu zinaonesha Iran ilisema uwongo wakati wa makubaliano ya nyukilia ya mwaka 2015.

Akitambulisha nyaraka hizo kwa njia ya televisheni hatua iliyoenda sambamba na kuonesha picha zilizorekodiwa katika mikanda ya vidio Netanyahu aliishutumu Iran kwa kudanganya kuhusiana  na mipango yake ya nyukilia  ingawa hakutoa ushahidi iwapo Iran ambaye ni adui  mkubwa wa Israel imekuwa ikiendeleza mipango ya kujipatia silaha za nyukilia hata baada ya makubaliano kati yake na mataifa sita yenye nguvu duniani.

 Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amekosoa madai hayo ya hivi karibuni na kumshutumu Netanyahu pamoja na rais wa Marekani Donald Trump ambaye Mei 12 mwaka huu anatarajia kufanya uamuzi wa kujiondoa au kusalia kwenye makubaliano hayo ya nyukilia na Iran.

 Mohammad Javad Zarif iranischer Außenminister (Getty Images/AFP/A. Kenare)

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif

Iran siku zote imekuwa ikikanusha kuwa na mipango ya kuwa na silaha za nyukilia na kusisitiza  kuwa mpango huo wa nyukilia ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Iran imemtaja Netanyahu kuwa muongo mkubwa.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pembezoni mwa rais wa Nigeria Muhammadu Buhari anayezuru nchini humo  Trump alisisitiza juu ya mapungufu yaliyoko kwenye mkataba huo akisema makubaliano hayo yatafikia kikomo chake katika kipindi cha miaka saba ijayo na baada ya hapo Iran itakuwa huru kuendelea na mipango yake ya nyukilia na pengine kuwa na silaha za nyukilia.

Wakati nchi nyingi zenye nguvu duniani zikisema makubaliano hayo kwa sasa yanafanya kazi vema kama ilivyokusudiwa na kuwa ni njia bora ya kuizuia Iran kutotengeneza bomu la nyukilia lakini bado rais Donald Trump kwa miezi kadhaa amekuwa akitishia kujiondoa.

Akizungumza mjini Tel Aviv  Netanyahu amesema katika hatua ya mafanikio makubwa kiinteligensia  hivi karibuni Israel ilijipatia makumi kwa maelfu ya nyaraka zinazohusiana na mpango wa nyukilia wa Iran ambazo imedai  mwaka 2017 zilihamishiwa kwenye  jengo moja mjini Tehran  ambalo kwa nje linaonekana kuchakaa.

Nyaraka hizo zimekabidhiwa kwa Marekani na pia zinatarajiwa kukabidhiwa kwa nchi kadhaa   na katika Shirika la Kimataifa la nguvu za Atomiki (IAEA).

Hayo yanajiri baada ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pamoja na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuondoka mjini Washinton juma lililopita pasipo mafanikio yoyote katika juhudi za kumshawishi rais Doanld Trump kuyanusuru makubaliano hayo ya nyukilia na Iran.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/DPAE

Mhariri: Caro Robi

 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com