Israel kuwasafirisha wahamiaji wa kiafrika hadi Uganda | Masuala ya Jamii | DW | 30.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Israel kuwasafirisha wahamiaji wa kiafrika hadi Uganda

Israel hivi karibuni ina mipango ya kuanza kuwarejesha barani Afrika wahamiaji takribani 50,000 kutoka Eriteria na Sudan.Inaaminika wahamiaji hao watapelekwa Uganda

Taarifa kutoka kwa waziri wa ndani wa Israel Gideon Sa'ar imesema hivi karibuni itaanza harakati za kuwarejesha barani Afrika wahamiaji ambao wengi waliingia nchini humo tangu mwaka 2006 kupitia Misri ambayo inapakana na Israel.

Israel inawaona wahamiaji hao kuwa wageni waliongia kinyume cha sheria, na inasema wameleta kero katika maeneo masikini nchini humo wakitafuta nafasi za kazi. Aidha Israel imepuzilia mbali msimamo wa mashirika ya kutetea haki za binadamu kuwa wengi wa wahamiaji hao wanatoroka makwao wakitafuta hifadhi ya kisiasa.

Sa'ar amesema kumeafikiwa makubaliano na taifa moja barani Afrika mbali na Eriteria na Sudan ambalo limekubali kuwahifadhi wahamiaji hao ambao hivi karibuni watatakiwa kuondoka kwa kile alichokitaja kwa hiari yao.

Wahamiaji kutoka Afrika wakisubiri kupata nafasi za kazi mjini Tel Aviv

Wahamiaji kutoka Afrika wakisubiri kupata nafasi za kazi mjini Tel Aviv

Inaaminika Uganda imekubali kuwapokea wahamiaji

Mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu wafanyakazi wa kigeni Michal Rozin ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kuwa Uganda ndiyo nchi iliyokubali kuwapokea wahamiaji hao waliokuwa wamefanya makaazi yao Israel.

Rozin wa kutoka chama cha mrengo wa shoto cha Mertz kinachopinga serikali ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu amesema kuna fununu kuwa Uganda huenda ilikubali mpango huo ili ipewe fedha na silaha.

Kufikia jana,maafisa wa serikali ya Uganda hawakuwa wamethibitisha madai hayo. Gazeti la Haaretz la Israel limeripoti bila kutaja jina la nchi yoyote kuwa nchi iliyokubali kuwachukua wahamiaji hao hivi karibuni ilikamilisha makubaliano ya kupewa silaha za kivita yakiwemo makombora na kusaidiwa kuboresha uwezo wa jeshi lake la anga.

Rozin amesema serikali imeingia katika makubaliano hayo lakini mkuu wa sheria wa Israel lazima atoe idhini yake ili mpango huo utekelezwe.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya bunge ameitaka serikali ya Israel kufichua maelezo zaidi kuhusu mpango huo yakiwemo iwapo kuna hakikisho kuwa wahamiaji hao hawatalazimishwa kuondoka Israel na kurejeshwa Sudan au Eriteria kwani wakirejeshwa katika nchini zao watahatarisha maisha yao.

Kurejeshwa kwa wahamiaji ni ukiukaji wa haki

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamesema Israel imewafunga jela mamia ya wahamiaji kutoka barani Afrika na imechukua hatua nyingine za kuwashinikiza kulazimika kuondoka nchini humo.

Raia wa Israel wakiandamana kuwaunga mkono wahamiaji wa kiafrika

Raia wa Israel wakiandamana kuwaunga mkono wahamiaji wa kiafrika

Kulingana na mratibu wa shirika la kutetea haki za binadamu linaloshughulikia sera za wafanyakazi wahamiaji Sigal Rozen,maelfu ya wahamiaji wanaaminika kuondoka nchini humo katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kupitishwa kwa sheria inayoruhusu kukamatwa kwa wahamiaji wasio na makaratasi rasmi ya kuishi Israel kufungwa jela hadi miaka mitatu.

Mwezi Julai,kundi la wa Eriteria 14 lilirejeshwa nchini kwao baada ya kupewa dola 1,500 kila mmoja na maafisa wa serikali ya Israel hatua ambayo shirika la kutetea haki za binadamu HMW ilitaja ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na kusema rekodi mbaya ya Eritrea kuhusu masuala ya haki za binadamu inatia wasiwasi.

Kundi jingine lilisafirishwa hadi Sudan kusini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na wengine wamepewa fedha kuondoka kwa hiari.Kiasi ya waafrika 2,000 wanazuiliwa katika vituo vya kuwazuia wahamiaji.

Uzio ulioimarishwa katika mpaka kati ya Israel na Misri katika eneo la Sinai,umepunguza kwa kiasi kikubwa kuingia kwa wahamiaji ambao walikuwa wakiingia Israel kwa kiwango cha hadi wahamiaji 2,000 kwa mwezi mwaka 2011.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters

Mhariri:Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com