1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yaridhishwa,Trump kuiondoa kwenye marufuku ya usafiri

6 Machi 2017

Iraq imeonesha kuridhishwa kwake na hatua ya rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa nchi hiyo kutoka kwenye orodha ya nchi alizozilenga katika marufuku ya usafiri kwenda Marekani.

https://p.dw.com/p/2YjKt
USA Donald Trump vor dem US-Kongress in Washington
Rais Trump kutoa marufuku mpya ya usafiriPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Martinez Monsivais

Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje ya taifa hilo ilisema, "Uamuzi huo ni hatua muhimu na unatilia nguvu zaidi ushirikiano baina ya Iraq na Marekani katika nyanja nyingi na hasa katika vita dhidi ya ugaidi ambapo Marekani iko katika mstari wa mbele."

Afisa mkuu wa ikulu ya Marekani Kellyane Conway, aliliambia shirika la habari la Fox, Trump anatarajiwa kutia saini amri mpya ya rais itakayopiga marufuku raia wa mataifa sita yenye idadi kubwa ya waislamu kuingia Marekani, baada ya jaribio lake la kwanza la marufuku kuzuiwa na mahakama hapo awali.

Conway alisema amri hiyo mpya ya rais, itaweka marufuku ya siku 90 ya raia wa Iran, Libya, Syria, Somalia, Sudan na Yemenkuingia nchini humo na itaanza kutimizwa Machi 16. Amezidi kueleza kwamba sababu kuu iliyopelekea kuondolewa kwa Iraq katika orodha hiyo ni kwa kuwa nchi hiyo iliyoko mashariki ya kat, imeanzisha mfumo mpya wa ukaguzi kama uchunguzi wa kina wa visa na kutoa data kwa Marekani, na pia kwa jinsi inavyoshirikiana na Marekani katika kupambana na wanamgambo wa kundi linalojiita Islamic State, IS.

Waliopata uraia kupitia green card hawatoathirika na marufuku mpya

Afisa huyo wa White House alisema amri hiyo mpya ya rais inahakikisha pia, maelfu ya watu waliopata uraia wa kudumu nchini Marekani kupitia green card, na wanaotoka mataifa hayo yatakayotajwa kwenye marufuku hiyo mpya, hawatoathirika na marufuku hiyo.

Schottland Proteste gegen Trump Muslim-Bann
Waandamanaji wakipinga marufuku ya awali ya TrumpPicha: Getty Images/M. Runnacles

Zaidi ya kesi 12 ziliwasilishwa mahakamani kupinga amri ya kwanza aliyoitoa Trump na jimbo la Washington lilifanikiwa katika juhudi zake za kutaka isitishwe na mahakama, kwa madai kwamba ilikiuka katiba kwa kuchochea ubaguzi wa kidini.

Trump aliwakashifu kadamnasi majaji waliotoa uamuzi wa kuisitisha hiyo amri yake ya awali na akaapa kuipeleka kesi hiyo katika mahakama ya juu zaidi, lakini baadae aliamua kuandika amri mpya yenye mabadiliko ambayo alihisi yatafanya iwe rahisi kwake kujitetea mahakamani iwapo amri hiyo itapingwa tena.

Amri itatolewa ili kuimarisha usalama

Kulingana na Conway, amri hii mpya ya rais haitoanza kutimizwa mara moja akidai sababu ya jambo hilo ni kuhakikisha hakuna mtafaruku unaozuka kwa baadhi ya wasafiri kama ilivyokuwa, ilipotolewa ile amri ya kwanza. Wakimbizi walio safarini na ambao wameidhinishwa, watakubaliwa kuingia Marekani.

USA Virginia Dulles Airport
Marufuku ya awali ilizua mtafaruku miongoni mwa wasafiri katika viwanja vya ndegePicha: DWP. Dadhania

Lakini afisa huyo vile vile alisema kwamba amri hiyo mpya itatolewa kwa msingi wa kuimarisha usalama wa Marekani na haitawekwa kwa lengo la ubaguzi wa kidini. Alisema, "Ni tofauti kabisa na ile ya kwanza kwa hali muhimu mno, itailinda nchi na kutuweka sote salama."

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/DPA

Mhariri: Saumu Yusuf