1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iheanacho awafunika Salah, Mahrez katika AFCON

Bruce Amani
12 Januari 2022

Kelechi Iheanacho aliwafunika wachezaji wenzake nyota wa Premier League Mohamed Salah na Riyad Mahrez jana wakati Nigeria iliandikisha mwanzo mzuri kwa kampeni yao ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika -AFCON

https://p.dw.com/p/45PLT
Fußball Africa Cup of Nations | Nigeria vs Ägypten | Mohamed Salah
Picha: Samuel Shivambu/BackpagePix/picture alliance

Mshambuliaji huyo wa Leicester City alifunga bao pekee kunako dakika ya 30 wakati Nigeria iliishinda Misri 1 – 0 katika mpambano wa miamba ya Kundi D katika mji wa kaskazini magharibi wa Garoua nchini Cameroon.

Bao lake la ushindi na mchezo wake kwa ujumla ulimpa Iheanacho tuzo ya mchezaji bora wa mechi katika siku ambayo mfungaji matata wa Liverpool Salah na winga wa Manchester City Mahrez walishindwa kutamba.

Ilikuwa mechi ya nane kuzikutanisha Misri na Nigeria katika mashindano hayo ya Afrika na mabingwa mara tatu Nigeria wameshinda mara nne na kutoka sare mbili.

Fußball Africa Cup of Nations | Algerien v Sierra Leone
Algeria ilibanwa na Sierra Leone katika Kundi EPicha: CHARLY TRIBALLEAU/AFP

Nigeria ilifanikiwa baada ya maandalizi yenye changamoto ambapo kocha Mjerumani Gernot Rohr alifutwa kazi kufuatia matokeo mabaya ya kufuzu Kombe la Dunia na nyota wa zamani wa timu ya taifa Augustine Equavoen akachukua majukumu kwa muda. Kikosi cha Equavoen kilikuwa bila ya washambuliaji Victor Osimhen, Emmanuel Dennis na Odion Ighalo kwa sababu kadhaa, lakini timu yake ilishambulia toka kipyenga cha mwanzo na kumfanya ajivunie.

Winga mwenye kasi Moses Simon alikuwa na mchango mkubwa wakati the Super Eagles walijiweka kifua mbele katika uwanja uliokuwa na mashabiki 30,000. Krosi yake ilizuiwa kwa sehemu na Ahmed Hegazy na Mnigeria Joseph Aribo akagonga kwa kichwa ukavurumishwa wavuni na Iheanacho.

Bahati nzuri; Misri itakutana na Misri na wapinzani ambao hawaonekani kuwa wagumu sana Guinea-Bissau na Sudan katika mechi zao zilizobaki na wana nafasi kubwa ya kutinga 16 za mwisho.

Algeria walipewa nafasi kubwa ya kushinda mechi ya ufunguzi ya Kundi E dhidi ya Sierra Leone, timu inayoorodheshwa nafasi ya chini mno na ambayo imeshiriki Afcon kwa mara ya kwanza tangu 1996.

Fußball Africa Cup of Nations | Sudan vs Guinea-Bissau
Guinea-Bissau walikosa penalti dhidi ya SudanPicha: DANIEL BELOUMOU OLOMO/AFP

Lakini nahodha Mahrez hakuweza kuipa msukumo timu yake katika mji wa bandari ya Atlantiki wa Douala na umahiri wa kipa wa Sierra Leone Mohamed Kamara aliyefanya kazi ya ziada na kupewa tuzo ya mchezaji bora wa mechi.

Ivory Coast, inayozingatiwa kuwa kitisho kikubwa kwa Algeria katika mashindano hayo, itakabana koo na Guinea ya Ikweta leo katika mechi inayotoa nafasi kwa timu zote kukamata usukani wa kundi lao. Sare hiyo imeiwezesha Algeria kurefusha rekodi yao ya kutopoteza mchezo katika mechi 35 mfululizo za mashindano hayo. Algeria itapambana na Guinea ya Ikweta Jumapili na Ivory Coast itakutana na Sierra Leone siku hiyo hiyo.

Katika mechi ya mwisho jana usiku ya Kundi D, kipa wa Sudan Ali Abou Achrine aliokoa penalty ya dakika za mwisho na kuhakikisha wanapata sare ya 0 0 Na Guinea Bissau mjini Garoua. Achrine aliipangua penalty hafifu ya kiungo Pele. Kipa huyo alirekebisha makosa yake na kuwa shujaa baada ya kumuangusha kwenye kijisanduku Steve Ambri na kusababisha penalti dakika nane kabla ya mechi kuisha.

afp, reuters, ap, dpa