Hillary Clinton arejea katika kampeni na kumshambulia Trump | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.09.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hillary Clinton arejea katika kampeni na kumshambulia Trump

Mgombea wa chama cha Democratic katika kinyan'ganyiro cha urais nchini Marekani Hillary Clinton amerejea tena katika kampeni na kutoa kauli ya tahadhari dhidi ya mpinzani wake Donald Trump.

Mgombea wa chama cha Democrats Hillary Clinton akiwahutubia wafuasi wake North Carolina

Mgombea wa chama cha Democrats Hillary Clinton akiwahutubia wafuasi wake North Carolina

Akizungumza katika mikutano miwili tofauti ya kampeni kwenye majimbo mawili, North Carolina na Washington, Hillary Clinton alisema amefurahi kurejea katika kampeni hizo baada ya hapo awali kushauriwa na madaktari kubakia nyumbani hadi atakapopata nafuu kutokana na maradhi ya homa ya mapafu yaliyokuwa yakimkabili.

Hali ya afya ya Hillary Clinton ilidhoofika wakati wa kumbukumbu ya mika 15 tangu yalipofanyika mashambulizi ya kigaidi nchini Marekani tarehe 11/9/ 2001.

"Ni jambo jema kuwa nimerejea katika kampeni" alisema mgombea huyo wa chama cha Democratic huku akishangiliwa na wafuasi wake alipohutubia katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Greensboro, North Carolina.

Hillary Clinton alitangaza kuendelea na mikutano ya kampeni katika majimbo ambayo mgombea wa chama cha Republican Donald Trump amekwishafanya mikutano yake ya kampeni ikiwa ni pamoja na jimbo la Florida ambalo kila mgombea anawania kulichukua.

Wakati suala la afya ya wagombea wote wawili likizua mjadala katika mikutano ya kampeni ya viongozi hao , Hillary Clinton alienda mbali zaidi kwa kutoa taarifa zinazohusiana na afya yake akisema ni mwenye afya njema na anaweza vema kutekeleza majukumu ya uongozi. Kwa upande mwingine wakati mgombea wa chama cha Republican Donald Trump akionekana kuwa na uzito mkubwa daktari wake alithibitisha kuwa mgombea huyo ana afya njema.

Hillary Clinton amshambulia Trump

Akizungumza katika mikutano hiyo ya kampeni Hillary Clinton hakusita kumshambulia kwa maneno Donald Trump kutokana na kauli ya awali aliyoitoa akikataa kusema iwapo ana amini kuwa Rais Barack Obama ni mzaliwa wa Marekani na pia kumkashifu mchungaji mwenye asili ya Afrika ambapo Trump alitembelea kanisa lake mjini Michigan wiki hii.

Kwa miaka kadhaa Donald Trump alikuwa akiendesha harakati akihoji kama Rais Barack Obama amezaliwa nchini Marekani na kutumia majukwaa kutangaza kuwa Rais huyo wa sasa wa Marekani alizaliwa nje ya nchi hiyo na kuwa hakusitahili kuwa Rais wa nchi hiyo kwa mujibu wa katiba ya Marekani.

Hapo jana wakati Trump alipohojiwa na gazeti la Washington Post iwapo ana amini kuwa Rais Obama alizaliwa mjini Hawaii, alishindwa kutoa jibu kwa mara nyingine akisema atajibu swali hilo wakati muafaka utakapowadia. Hata hivyo taarifa iliyotolewa baadaye na waratibu wa mikutano ya kampeni ya mgombea huyo ilisema Trump ana amini kuwa Rais Obama alizaliwa nchini Marekani.

" Baada ya kufanikiwa kupata cheti cha kuzaliwa cha Rais Barack Obama wakati wengine wameshindwa , Donald Trump sasa ana amini kuwa Rais Obama ni mzaliwa wa Marekani " ilisisitiza taarifa hiyo.

Aidha mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton alisema kitendo cha Trump kumshambulia mchungaji kinazidi kumnyima sifa Trump za kuwa Rais wa nchi hiyo na kuwataka wapiga kura kumkataa wakati wa uchaguzi wa mwezi Novemba.

Mwandishi : Isaac Gamba/ DPAE/ ECA

Mhariri :Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com