Hamas: hatutaitambua Israel | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 22.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Hamas: hatutaitambua Israel

Kimyume na matamko ya Rais wa zamani Jimmy Carter Hamas imesema imekubali kuundwa kwa taifa la wapalestina na wala haijakubali kuitambua Israel

Kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal akiwa mkutanoni na waziri wa nchi za nje wa Saudi Arabia Faisal

Kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal akiwa mkutanoni na waziri wa nchi za nje wa Saudi Arabia Faisal

Chama cha Hamas limeeleza dhahiri kwamba haliko tayari kutambua Taifa la Israel.


Kiongozi wa kundi hilo Khaled Meshaal amesema Hamas imekubali kuhusu kuundwa kwa taifa la Palestina katika ardhi ya Jerusalem Mashariki, ukingo wa magharibi na Gaza lakini haijasema kwamba italitambua taifa la Israel.


Kauli hiyo ya Hamas inafuatia matamko ya Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter aliesema chama hicho kiko tayari kuitambua Israel.


Baada ya Carter kukutana mara mbili na Meshaal mjini Damascus mwishoni mwa wiki Rais huyo wa zamani alisema. "Wamesema kwamba watakubali kuundwa kwa taifa la Palestina katika mipaka ya mwaka wa 1967 iwapo hatua hiyo itakubaliwa na wapalestina na pia watakubali kuishi na taifa la Israel kama majirani kwa amani"


Carter alikuwa anaongea kuhusu maeneo ya Ukingo wa magharibi na ukanda wa Gaza pamoja na kura ya maoni ambayo Marekani inatarajia wapalestina wataifanya kwa minajili ya kupata amani ya mashariki ya kati mwaka huu.


Afisa mmoja wa kundi la Hamas Sami Abu Zuhri amesema wakimbizi wa Palestina wanaoishi uhamishoni wanatakiwa kushiriki katika kura hiyo. Jambo ambalo huenda likapingwa na Israel kwani nchi hiyo inahofia kurejea kwa wapalestina wengi katika ardhi ambayo sasa inaimiliki.


Lakini Meshaal ambaye Carter anataka ajumlishwe katika mazungumzo ya amani yanayoendelea kati ya Rais wa Palestina Mahmoud ABBAS na Israel, amesema Hamas itaheshimu matakwa ya wapalestina hata yakienda kinyume na imani ya kundi hilo.


Kiongozi huyo amesema iwapo Israel itaondoka katika mipaka ambayo nchi hiyo ilinyakuwa katika vita vya mashariki ya kati mwaka wa 1967 basi Hamas itasitisha mashambulio dhidi ya wayahudi kwa kipindi cha miaka kumi.


Lakini kiongozi wa pili katika kundi la Al Qaida Ayman

al-Zawahiri amesema anashangazwa na mpango wa Hamas wa kuingia katika amani na Israel chini ya misingi ya kura ya maoni ya wapalestina. Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Internet Al-Zawahiri amesema hatua hiyo ni kinyume na sheria ya kiislamu.


Kwengineko Israel imesema ziara ya Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter mashariki ya kati kwa nia ya kutafuta usitishswaji wa mashambulio imeambulia patupu.


Afisa mmoja wa ngaza za juu katika wizara ya usalama nchini humo Amos Gilad amesema kundi la Hamas halikutoa chochote kipya katika masharti yake lilipokutana na Carter.


Hapo jana Carter aliongea na kiongozi wa Hamas Meshaal kwa njia ya simu na kumuomba asitishe mashambulizi dhidi ya wayahudi angalau kwa mwezi mmoja bila kutoa masharti yoyote lakini ombi lake likagonga mwamba licha ya wawili hao kukutana kwa zaidi ya masaa saba mwishoni mwa wiki.


Wakati huo huo Marekani ambayo imekataa kukimjumlisha chama cha Hamas katika mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati imesema haijaona mabadiliko yoyote katika misimamo ya chama hicho.


Baada ya ziara yake ya mashariki ya kati Carter amesema ameelewana na Hamas kuhusu kura ya maoni itakayopelekea maelewano kati ya kundi hilo na lile la Fatah linaloongozwa na Abbas.


Hamas iliteka eneo la ukanda wa Gaza kutoka mikononi kwa Fatah lakini kiongozi wa Fatah Mahmoud Abbas anataka eneo hilo lirejee mikononi mwa uongozi wa kundi lake.


Carter, ambaye alisaidia kurejesha amani kati ya Israel na Misri mwaka wa 1979 anapinga hatua ya Marekani, Israel na Jumuia wa Ulaya ya kutoshirikisha Hamas katika mpango wa amani ya mashariki ya kati.


Israel iliondoa wanajeshi na wayahudi katika ukanda wa Gaza mwaka wa 2005 lakini bado inashikilia mipaka ya eneo hilo na imeongeza masharti katika mipaka hiyo tangu Hamas ilipochukua uongozi wake.

 • Tarehe 22.04.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DmCn
 • Tarehe 22.04.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DmCn
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com