Hali ya Tahadhari Yatangazwa Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Hali ya Tahadhari Yatangazwa Ukraine

Hatua za usalama zimeimarishwa Ukraine kuelekea maadhimisho ya ushindi wa Urusi katika vita vikuu vya pili vya Dunia huku waziri mkuu wa Ukraine akisema haamini kama matamshi ya rais Vladimir Putin wa Urusi ni ya dhati.

Sherehe za Siku ya Ushindi katika mji wa Luhansk,mashariki ya Ukraine

Sherehe za "Siku ya Ushindi "katika mji wa Luhansk,mashariki ya Ukraine

Mod:

Serikali ya Ukraine imeimarisha hatua za usalama kuelekea sherehe za leo za kuadhimisha ushindi wa Urusi katika vita vikuu vya pili vya dunia.Wakati huo huo waziri mkuu wa Ukraine anaséma haamini kama matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na rais Vladimir Putin wa Urusi ni ya dhati.Zaidi anasimulia Oummilkheir.

"Nimeingiwa na wasi wasi kutokana na taarifa ya Vladimir Putin.Wanachokisema sio wanachokitenda" amesema waziri mkuu wa ukraine Arseniy Yatsenuk kupitia kituo cha televisheni cha nchi hiyo na kuamuru wakati huo huo hatua za usalama ziimarishwe.

Jumatano iliyopita rais Vladimir Putin aliushangaza ulimwengu alipowatolea wito wanamgambo wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki la Ukraine waakhirishe kile kinachotajwa kama kura ya maoni waliopanga kuitisha mwishoni mwa wiki hii na kuunga mkono wakati huo huo uchaguzi wa rais wa may 25 ijayo.Hata hivyo waasi wanaoshikilia zaidi ya miji 10 mashariki ya Ukraine wanaonyesha kuupuuza wito huo na kudhamiria kuitisha kura hiyo ya maoni.

Katika maeneo ambayo kura hiyo ya maoni imepangwa kuitishwa,baadhi ya wananchi wanalalamika :

O-Ton Olga Rukhmakova (W)

Watu hawataki pafanyike mageuzi kinyyume na matakwa yao.Wanahisi hakuna aliyewauliza maoni yao"

Kinyume na jinsi sherehe za kijeshi kuadhimisha "siku ya Ushindi" dhidi ya utawala wa wanazi mnamo mwaka 1945 zilivyokuwa katika uwanja mwekundu mjini Moscow,mjini Kiev sherehe hizo zimefanyika katika hali ya tahadhari ili kuepusha uchokozi.

Mkuu wa serikali ya jiji la Kiev amepiga marufuku mikusanyiko ya watu hadharani au gwaride kwa hofu mashujaa wa vita vikuu vya pili vya dunia wasije wakashambuliwa na wafanyafujo.

Rais wa mpito wa Ukraine Oleksanadr Turchynov amewataka wananchi katika kila pembe ya nchi hiyo wawe macho."Vizuwizi vimewekwa majiani mjini Kiev ambako ukaguzi wa kina unafanyika-kwasababu ya hofu wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi wasije wakafanya fujo" amesema rais wa mpito Oleksandr Turchynov na kuongeza sio tu mjini Kiev,lakini katika kila pembe ya Ukraine watu wanabidi wawe katika hali ya tahadhari."

Serikali ya Ukraine imeahidi kuendelea na opereshini dhidi ya magaidi katika eneo la Donetsk.Opereshini hizo zilizoanza ijumaa iliyopita zimeshaangamiza maisha ya dazeni kadhaa za watu.

Katika wakati ambapo katibu mkuu wa jumuia ya Usalama na ushirikiano barani Ulaya Lamberto Zannier anatarajiwa kuwasili Kiev hii leo, rais wa baraza la ulaya Herman Van Rompuy anapanga kufika katika mji mkuu huo wa Ukraine jumatatu ijayo kwa kile alichokitaja kuwa "kuonyesha uungaji mkono wa umoja wa ulaya kwa Ukraine kabla ya uchaguzi wa rais May 25 ijayo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com