1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ngumu kwa wanajeshi wa Ukraine walioko mashariki

Tatu Karema
16 Februari 2024

Kamanda wa majeshi ya Ukraine katika mji wa mashariki wa Avdiivka, Tarnavskyi Oleksandr, anasema wanajeshi wanaoulinda mji huo wako kwenye hali ngumu kutokana na mashambulizi makali ya wanajeshi wa Urusi.

https://p.dw.com/p/4cT4W
Ukraine | Vita | Volodymyr Zelensky na Oleksandr Syrsky
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine (kulia) akizungumza na kamanda wa jeshi la nchi hiyo, Oleksandr Syrsky.Picha: Ukrainian Presidential Press Off/ZUMAPRESS/picture alliance

Tarnavskyi alisema siku ya Ijumaa (Februari 16) kuwa mapigano makali yalikuwa yanaendelea mjini humo na wanajeshi wake walikuwa wnatumia nguvu zao zote na raslimali zilizoko kukabiliana na vikosi vya Urusi.

Kamanda huyo alisema ukweli ni kuwa hali ni ngumu, ingawa bado walikuwa wanaendelea kuudhibiti mji huo.

Soma zaidi: Putin asema hawezi kushindwa na Ukraine

Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, Tarnavskyi alisema wanajeshi hao wa Ukraine "wanapambana katika mazingira mabaya ya kibinaadamu na vikosi hasimu vinatumia nguvu kubwa" kwa maana ya wapiganaji, magari ya kivita na ndege kuelekea Avdiivka.

Katika uchambuzi wake siku ya Alhamis, Taasisi ya Utafiti wa Vita ya Marekani (ISW) ilisema kuwa wanajeshi wa Urusi wamesonga mbele katika uwanja wa vita kutokea pande mbalimbali.