1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gavana ashambuliwa siku chache kabla ya uchaguzi Nigeria

Sekione Kitojo
14 Februari 2019

Watu watatu wameuwawa baada ya magaidi wa itikadi kali ya Kiislamu  kuushambulia msafara  wa  gavana nchini Nigeria, siku kadhaa  kabla  ya  nchi  hiyo  kufanya uchaguzi  wa  rais siku  ya Jumamosi.

https://p.dw.com/p/3DOqz
Vor Wahlen in Nigeria  Muhamadu Buhari (M), Präsident von Nigeria, und Atiku Abubakar (r)
Picha: picture-alliance/AP/B. Curtis

Wakati  huo  huo, chama  kikuu  cha  upinzani  cha  Nigeria kimedai  kwamba tume  ya  uchaguzi imekuwa  na  zaidi  ya  wapiga  kura milioni  moja  hewa  katika  daftari la  wapiga  kura.

Wanachama  wa  kundi  linalojiita  Dola  la  Kiislamu la kanda  ya  Afrika  Magharibi  wamedai  kuhusika  na shambulio  la  jana  dhidi  ya  msafara  wa  Kashim Shettima, gavana  wa  jimbo  la  kaskazini  mashariki  la Borno, na  kusababisha  watu 42  kuuwawa: Hayo ni kwa mujibu  wa  kundi  linalofanya  utafiti  wa  kijasusi  la marekani  SITE Intel.

Ofisi  ya  Shettima,  ambayo  msafara  wake  ulishambuliwa wakati  wa  mkutano  wa kampeni  karibu  na  mji  wa Dikwa,  kabla  ya  uchaguzi  utakaofanyika  nchi  nzima Februari  16, hata  hivyo  imethibitisha   kuuwawa  kwa watu  watatu.

Mjumbe  wa  kundi  la  walinzi  wa  umma  katika  eneo hilo, lililoudwa  ili  kulinda  vijiji  katika  jimbo  la  Borno dhidi  ya  ugaidi, amesema  watu  kadhaa  wamekamatwa wakati  wa  shambulio  hilo  la kushitukiza.

Nigeria Kashim Shettima, Gouverneur Borno
Gavana wa jimbo la Borno Kashim ShettimaPicha: Reuters/A. Sotunde

"Raia  wawili  pamoja  na  mwanajeshi  mmoja  waliuwawa papo  hapo, wakati  watu  wenye  silaha  waliondoka  na magari  manane,"  aliliambia  shirika  la  habari  la Ujerumani  dpa  kwa  masharti  ya  kutotajwa  jina.

"Baadhi  ya  watu  katika  msafara  huo  waliwakamatwa mateka  na  kuondoka  nao,"  ameongeza.

Ukaguzi wa daftari ya wapiga kura

Wakati  huo  huo mwenyekiti  wa  chama  cha  upinzani cha  Peoples Democratic Party, PDP Uche Secondus, amesema  katika  mkutano  na  waandishi  habari  mjini Abuja  kwamba  tume  ya  uchaguzi  nchini  humo, haikufanya  ukaguzi  wa  daftari  la  wapiga  kura, kabla  ya kuchapisha  majina  ya  wapiga  kura.

"Maelezo  ambayo  si  mazuri  yamejitokeza, moja  kati  ya njia  za  wizi  wa  kura , ni kutoweka  rekdi  halisi  ya  daftari ya  wapiga  kura  na  kwa  hiyo  si  rahisi  kuamini  ukuaji wa  demokrasi  na  taifa  kwa  jumla, amesema  mwenyekiti huyo.

Nigeria Rivers State | Wahlkampf Muhammadu Buhari, Präsident
Rais Muhammadu Buhari (kulia)katika mkutano wa kampeni wa chama chake Picha: Reuters/Nigeria Presidency/Bayo Omoboriowo

Pia  amedai  kwamba kulikuwa  na  utaratibu  ulioratibiwa wa  kuandikisha  watu  wa  mataifa  ya  kigeni kuwa  wapiga kura katika  uchaguzi  huo.

Chama  cha  Peoples Democratic Party, ambacho mgombea  wake  wa  kiti  cha  urais  ni  Atiku Abubakar, ni chama  kikuu  cha  upinzani  nchini  Nigeria. Madai  ya wapiga  kura  hewa  yanaelekea  kuzusha  wasi  wasi katika  kile  ambacho  kinaonekana  kuwa  ni mpambano utakaotoa  matokeo  ya  karibu  kati  ya  Abubakar, makamu wa  rais  wa  zamani , na  rais Muhammadu  Buhari.

Tume  ya  uchaguzi  imesema  watu  milioni  84 wameandikishwa  kupiga  kura  katika  nchi  hiyo  yenye wakaazi  milioni  190.

Msemaji  wa  tume  ya  uchaguzi  hakupatikana  kutoa maelezo.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ap / dpa

Mhariri: Grace Patricia Kabogo