1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan: Umoja wa Ulaya utende haki mvutano na Ugiriki

7 Septemba 2020

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameutolea mwito Umoja wa Ulaya kutoegemea upande wowote katika mvutano unaozidi kutokota juu ya uchimbaji Mafuta katika eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterenia.

https://p.dw.com/p/3i6Wj
Türkei Recep Tayyip Erdogan Erdgas Fund Mittelmeer
Picha: picture-alliance/dpa/Turkish Presidency

Katika mazungumzo kwa njia ya simu, rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel amesisitiza umuhimu wa kupunguza mzozano na kuitaka Uturuki kujizuia katika shughuli zake ambazo zinachochea mvutano huo na hasimu wake Ugiriki.

Utafutaji wa Mafuta na gesi unaofanywa na Uturuki katika eneo la maji linalodaiwa kumilikiwa na mwanachama wa Umoja wa Ulaya Ugiriki, mara kadhaa umetia doa uhusiano baina ya wanachama hao wawili wa Jumuiya ya kujihami NATO na kuiweka Ankara katika upinzani dhidi ya muungano wa ulaya.


Mzozo huo unaozidi kuongezeka kila kukicha unatarajiwa kuwa ajenda itakayotawala mazungumzo ya baraza la Umoja wa Ulaya baadaye mwezi huu, huku baadhi ya wanachama wakishinikiza Uturuki iwekewe vikwazo.


Wakati wa mazungumzo ya kwenye simu, kiongozi wa Uturuki ameitaka taasisi hiyo ya "Umoja wa Ulaya na nchi wanachama kutenda haki, kutoegemea upande wowote na kuwa na uwajibikaji katika masuala ya kikanda hasa eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterenia," imesema ofisi ya rais.

Mwezi uliopita Uturuki ilipeleka meli yake ya utafiti ya Oruc Reis katika maji yaliyoko kati ya Ugiriki na Cyprus, hali iliyosababisha Ugiriki kufanya mazoezi ya jeshi la wanamaji kwa ajili ya kulinda mipaka yake ya majini.

Hapo Jumamosi, Erdogan aliionya Ugiriki kwamba"ama watapaswa kuelewa lugha ya siasa na diplomasia au kupitia uzoefu mchungu".

Mwanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel alitarajiwa kuliibua suala la vikwazo dhidi ya Uturuki katika mkutano unaokuja lakini hadi sasa Ufaransa, ambayo imetuma ndege za kivita katika ukanda huo kuisaidia Ugiriki, haijaweza kuyashawishi mataifa ya Umoja wa Ulaya kuungana nayo katika msimamo wake mkali.

Michel amemueleza Erdogan kwamba hatua zote zitazingatiwa katika mkutano unaokuja. Erdogan naye amejibu akisema mbinu zinazotumiwa na Umoja wa Ulaya katika suala hilo itakuwa ni jaribio la uaminifu kwa sheria za kimataifa na amani ya kikanda na kuongeza kuwa hatua za uchochezi zilizochukuliwa na baadhi ya wanasiasa wa Ulaya hazitoi suluhisho.

Wakati mvutano ukizidi kuwa mkubwa, vikosi vya Uturuki siku ya Jumapili vilianza mazoezi ya kila mwaka yaliyopewa jina la "dhoruba ya Mediterenia" katika eneo la Uturuki la Cyprus Kaskazini linalotambulika na Uturuki pekee.

Mvutano kati ya Uturuki na Ugiriki unahusu haki za kutafuta na kuchimba mafuta na gesi katika eneo linalozozaniwa katika bahari Mediterrania
Mvutano kati ya Uturuki na Ugiriki unahusu haki za kutafuta na kuchimba mafuta na gesi katika eneo linalozozaniwa katika bahari MediterraniaPicha: AFP/Greek defence ministry


Kisiwa cha Cyprus kimegawanyika baina ya udhibiti wa Ugiriki katika eneo la kusini na udhibiti wa Uturuki eneo la kaskazini.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi
Mhariri: Josephat Charo