Dalai Lama asisitiza kuwa yuko tayari siku zote kukutana na China. | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Dalai Lama asisitiza kuwa yuko tayari siku zote kukutana na China.

Kiongozi wa Kidini wa Watibet, Dalai Lama amesema wakati wote yuko tayari kukutana na uongozi wa China, hususa Rais wa nchi hiyo Hu Jintao kufuatia ghasia za Tibet, iwapo China ingekuwa tayari kwa hilo.

Kiongozi wa kidini wa Tibet, Dalai Lama.

Kiongozi wa kidini wa Tibet, Dalai Lama.

Dalai Lama, aliwaambia wana habari kwamba siku zote, yuko tayari kukutana na viongozi wa China, licha ya kukiri kuwa kwenda Beijing kwa sasa, sio uamuzi wa busara.

Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel amewataka pia viongozi duniani, kusaidia kuweza kutatua suala hilo la Tibet.

Kiongozi huyo wa kidini wa Tibet pia, alielezea wasiwasi wake wa kutokea madhara kadhaa, wakati majeshi ya China yakidhibiti waandamanaji huko Tibet.

Katika hatua nyingine, Watibet 18 wameuawa na polisi wenye hadhi ya kijeshi, katika jimbo la Sichuan lililoko kusini magharibi mwa China, wakati ambapo serikali ya nchi hiyo imetoa ripoti yake kuhusiana na ghasia hizo katika eneo hilo bila kutaja shutuma hizo za polisi kufyatulia risasi waandamanaji wa kitibeti.

Watibeti 13 akiwemo mtoto wa miaka minane, wameuawa kwa kupigwa risasi katika ghasia hizo zilizotokea katika mji wa Aba, kwenye jimbo hilo la Sichuan ijumaa iliyopita na wengine watano waliuawa siku ya Jumamosi.

Chanzo kimoja cha habari kililiambia Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, kwamba malori saba yaliyokuwa yamepakia polisi jeshi hao, yaliingia katika mji huo wa Aba siku ya Jumanne.

Chanzo hicho cha habari kimearifu kuwa, Polisi jeshi hao walikuwa wakihoji watu waliokuwa wakijaribu kutoka muda wa usiku, pamoja na Watibet wowote waliokuwa wakitembea mtaani kwa makundi ama zaidi ya watu wawili.

Jana jioni serikali ya nchi hiyo ilitoa ripoti yake hiyo ya kwanza kuhusiana na ghasia za waandamanaji katika mji huo wa Aba na maeneo mengine ya jimbo la Sichuan na katika jimbo la jirani la Gansu kufuatia ghasia zilizotokea wiki iliyopita mjini Lahasa, Tibet.

Shirika la Habari la China liliarifu kuwa mamia ya waandamanaji walivamia ofisi za serikali, vituo vya polisi na shule katika mji huo wa Aba na kuanza kuiba vitu na kuchoma moto maduka katika mji huo, huku maafisa wengi wa polisi na wa serikali wakijeruhiwa.

Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba bendera ya serikali ya Tibet iliyoko uhamishoni wanadaiwa kutamka maneno yaliyosema ''uhuru wa Tibet'' pamoja na kubeba mabomu yaliyotengenezwa kwa petroli.

Mbali na kutoa taarifa za polisi wanane na wafanyakazi watatu wa serikali kujeruhiwa, ripoti hiyo haina taarifa ya majeruhi miongoni mwa waandamanaji.

Hata hivyo serikali ya China imekanusha kuwafyatulia risasi waandamanaji mjini Lhasa.

Kwa ujumla kumekuwa na taarifa tofauti zinazotolewa kati ya serikali ya China na Watibet kuhusiana na watu waliouawa tangu kuanza kwa ghasia hizo kufuatia maandamano yaliyoanza Machi 10 iliyokuwa kumbukumbu ya serikali ya Uchina kupinga harakati za kujitenga.


 • Tarehe 20.03.2008
 • Mwandishi Nyanza, Halima
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DRgq
 • Tarehe 20.03.2008
 • Mwandishi Nyanza, Halima
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DRgq
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com