1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto za dunia kutawala mkutano wa Umoja wa Mataifa

Yusra Buwayhid
24 Septemba 2019

Viongozi wa dunia Jumanne wanakutana katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Watajadili jinsi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, mizozo ya kikanda na mzozo unaoweza kutokea Mashariki ya Kati kuiathiri dunia nzima.

https://p.dw.com/p/3Q8Jc
USA UN-Generalversammlung in New York
Picha: picture alliance/dpa/D. Kalker

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ataufungua mkutano huo mkuu kwa hotuba itakayoeleza hali halisi ya ulimwengu kwa sasa. Atafuatiwa na msemaji wa kwanza kijadi - Brazil, ambayo mara hii inawakilishwa na rais wake mpya, Jair Bolsonaro- na Marekani ambayo itawakilishwa na Rais Donald Trump.

Mkutano huo unafanyika katika wakati ambapo kuna mivutano mikali kati ya Iran na Saudi Arabia inayoungwa mkono na mshirika wake wa miaka mingi - Marekani. Saudi Arabia inadai Iran imehusika na mashambulizi dhidi ya vituo vyake vya mafuta mapema mwezi huu, madai ambayo Iran inayakana.

Serikali ya Trump na ya Iran,  hivi karibuni zimekuwa zikitupiana maneno makali pamoja na vitisho. Marekani imeiongezea vikwazo Iran.

Rais wa Iran Hassan Rouhani, ambaye ameshawasili mjini New York Marekani, anatarajiwa kuzungumza mbele ya viongozi wa dunia hapo kesho."Ujumbe wa Iran kwa ulimwengu ni "amani na utulivu," amesema Rouhanni wakati alipowasili nchini Marekani, kulingana na taarifa za shirika la habari la serikali la Iran, IRNA.

USA | Trump kündigt Initiativen zur Religionsfreiheit während der UN an
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Rais wa Marekani Donald Trump na Makamu wa Rais Mike Pence.Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/E. Vucci

Idadi ya wanaohudhuria yaongezeka

Mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoanza Jumanne na kumalizika Septemba 30, umekusanya viongozi wa nchi 136 kati ya nchi wanachama wa umoja huo 193. Kuhudhuria huko kwa wingi ni ishara ya kuongezeka wasiwasi wa kutaka kuyashughulikia matatizo ya kiulimwengu ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na kitisho dhidi ya amani na utulivu.

Nchi zingine zitawakilishwa na mawaziri au makamu wa rais - isipokuwa Afghanistan, ambayo viongozi wake wamo katika harakati za kampeni za uchaguzi wa rais utakaofanyika Septemba 28, na Korea Kaskazini, ambayo badala ya kutuma waziri huenda ikatuma balozi wake katika Umoja wa Mataifa.

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wameahirisha mipango yao ya kushiriki katika mkutano huo, badala yake wametuma mawaziri.

Wiki iliyopita, Guterres amerudia tena onyo kwamba mivutano inazidi kupamba moto. Amesema  ulimwengu unakabiliwa na hali mgumu katika kila upande, hali ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la kukosekana kwa usawa miongoni mwa binadamu, ongezeko la chuki na kutovumiliana pamoja na idadi kubwa ya kutisha ya changamoto za amani na usalama.

Soma zaidi: Vijana waandamana kabla ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi