1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema yawaamuru wafuasi wake kumsaka Mbowe

21 Julai 2021

Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania CHADEMA, kimewaamuru wanachama na wafuasi wake kuingia mtaani kumsaka Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, kikidai kuwa hawajui yuko wapi na ana hali gani.

https://p.dw.com/p/3xmb3
Pressebilder von Chadema Press | Tansania Chadema-Partei
Picha: Chadema Press

Katibu Mkuu wa Chama hicho, John Mnyika mbele ya waandishi wa habari anatoa tamko hilo, ikiwa tayari imepita zaidi ya saa 10 Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe pamoja na baadhi ya watendaji wengine wasiopungua watano, kudaiwa kukamatwa na kushikiliwa na Jeshi la Polisi, Mjini Mwanza huku kukiwa hakuna maelezo ya kutosha kwa chama hicho cha upinzani kilichoibeba ajenda ya kudai Katiba mpya hadharani kwa kuendesha makongamano ya ndani nchi nzima. 

Mnyika amesema jitihada za chama hicho kujua mwenyekiti na watendaji wanaoshikiliwa wapo wapi zimeambulia patupu hivyo mkutano wa ndani wa chama chake umeamua kuwatangazia wanachama na wafuasi kutumia kila aina ya namna ili kumsaka kiongozi wao ambaye alifika Jijini Mwanza ili kuongeza shinikizo la kudai Katiba mpya katika kongamano la ndani lililozuiwa na Jeshi la Polisi kwa mara ya pili sasa.

Anführer von Tansanias Oppositions-Partei Chadema
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe Picha: DW/E. Boniphace

Chama hicho ambacho kiliambulia Jimbo moja katika Uchaguzi Mkuu uliopita walioushutumu kukiuka sheria na haki za binadamu, kimepeperusha lawama zake kwa Serikali Kuu kuhusika katika kuzima moto wake wa madai ya Katiba mpya kwa kuwa Mamlaka iliyopo hivi sasa imeweka wazi kwamba itahitaji muda ili kuendelea na mchakato wa Katiba mpya hii ni baada ya miito kila kona ya kudai kuendelezwa kwa mchakato wa Katiba mpya iliyosheheni maoni ya wananchi.

Aidha CHADEMA kimeitisha mkutano wa dharura wa Kamati Kuu ili kujadili kwa kina haya waliyoyatafsiri ni ukiukwaji wa haki ya kujumuika kisiasa kikiwataka wadau wote wa demokrasia na haki za binadamu kutofumbia macho kitendo hicho kilichofanywa na Jeshi la Polisi kwa kupaza sauti kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua stahiki.

Hadi sasa mamalaka jijini mwanza ambako mwenyekiti  Mbowe anadaiwa kukamatwa haijatolea ufafanuzi hoja za CHADEMA

Pressebilder von Chadema Press | Tansania Chadema-Partei
Wanachama wa Chadema wakati wa kongamano la kudai katibaPicha: Chadema Press

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaunga mkono kauli ya Rais Samia kwani amelipokea Taifa katika wakati ambao haukutarajiwa na sasa anatekeleza yale ya mtangulizi wake huku wakishauri hoja hiyo kuamshwa katika awamu yake ya pili, lakini ajenda hii inapuuziliwa mbali na baadhi ya vyama vya siasa kwa hoja kuwa bila Katiba mpya hawatashiriki uchaguzi wa 2025. 

DW ilizungumza kwa njia ya simu na mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Mwanza, Tanzania, Said Msonga juu ya suala hilo na akasema "nadhani ni jambo la mgongano wa kisheria zaidi kwa maana ya kwamba jeshi la polisi ambalo lina wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa watu na mali zao na chama cha demokrasia na maendeleo Chadema ambacho nacho kina haki y akufanya shughuli zake za kisiasa kwa mujibu wa sheria"

Itakumbukwa kwamba CHADEMA inapata nguvu ya kudai Katiba Mpya kutokana na wasifu wa Rais Samia kuwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba mwaka 2014 hivyo imani ya wengi ilileta mwangaza wa kuendelea kwa mchakato huo uliokwama kwa takribani miaka sita sasa, hii ni kutokana na mtangulizi wake Hayati John Magufuli kuweka wazi msimamo wake kwamba Katiba mpya si kipaumbele chake lakini hata hivyo Rais Samia pia ameomba apatiwe muda katika hili.